“RAIS William Ruto jana alisema kuwa japo Mlima Kenya unaonekana kuwa mgumu katika juhudi zake za kuchaguliwa tena mwaka wa 2027, anaamini kwa uwezo wa Mungu, hatimaye “utalegea” na kumsaidia kupata ushindi. “Ninajua kuna changamoto nyingi, kazi nyingi inapaswa kufanyika na mambo mengi yanahitaji kurekebishwa, lakini kwa maombi hata hali ngumu zaidi inaweza kuwa rahisi,” alisema. Rais alisema hatachoka kusaka uungwaji mkono eneo hilo, yeye binafsi na kupitia kwa washirika wake, akisema ana ahadi na wakazi wa Mlima Kenya aliowasifu kama “watu wenye busara wanaoweza kusoma barua hata kabla haijafunguliwa”. Ruto alizungumza katika Kaunti ya Murang’a alipohudhuria ibada katika Kanisa la African Inland Church (AIC) Githumu, Kandara, ikiwa ziara yake ya pili katika kaunti hiyo ndani ya wiki moja. Alisema yeye ndiye rais wa pekee nchini ambaye amejikita katika ujenzi wa masoko, viwanja vya michezo, nyumba za makazi na mabweni kwa wanafunzi, akisisitiza kuwa bado anajiona mshirika wa wapigakura wa Mlima Kenya. Rais aliongeza kuwa serikali yake inalenga kuweka fedha mikononi mwa wananchi kupitia sekta ya kilimo na miradi ya maendeleo, akisema anatekeleza ahadi zake za kampeni za mwaka wa 2022. Alipuuza madai ya upinzani kuhusu usalama akisema serikali yake imejitolea kulinda kila mwananchi licha ya “siasa za chuki na uzushi”. Rais Ruto alisema serikali za awali zilichelewesha maendeleo, hali ambayo serikali yake inalazimika “kurekebisha”. Alisisitiza kuwa fedha za mgao zinafika shuleni kwa wakati, akiwashutumu wanasiasa wanaoeneza “maneno ya kupotosha”. Kuhusu mzozo wa afya kupitia Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA), Rais alisema mfumo huo unafanya kazi vizuri na serikali inalipa madeni ya sekta ya afya. “Ninapigwa vita kupitia ukabila, uongo na matusi, lakini nitaendelea kuweka rekodi ya maendeleo yangu,” alisema. Kauli yake ilijiri siku chache baada ya kulalamika kuwa eneo lake la Rift Valley halijasajili wapigakura wengi, akisema atategemea maeneo mengine kumsaidia kushinda 2027. Waziri wa Ardhi Alice Wahome alisema kikosi cha kampeni tayari kimeundwa Mlima Kenya kuhakikisha Rais Ruto anapata ushindi 2027. Mbunge wa Githunguri Gathoni Wamuchomba na Mbunge Maalum Sabina Chege walionekana kumuunga Rais, wakisema amefanya kazi akiwalenga wananchi wa kawaida. Bi Chege alisema kwamba ingawa hakumuunga Rais katika uchaguzi wa 2022, sasa atamuunga mwaka 2027. “Ninyi ndio mliokuwa mkiimba kwamba mtaamka asubuhi na mapema kumpigia kura. Kanisa na uongozi wake tulipambana nao tukiwa upinzani wakisema Ruto anamtumikia Mungu aliye hai na si uchawi. Ninajiuliza kama huyo Mungu mliyemtumia kumuunga mkono Dkt Ruto amebadilika,” alisema. Bi Wamuchomba, alisema anajutia kujiunga na upinzani kumpinga Rais Ruto. “Ilifika mahali nikagundua nilikuwa mpumbavu. Haikuwezekana kuendelea kujifanya sioni masoko yakijengwa, nyumba za bei nafuu na bei ya kahawa kupanda kutoka Sh60 hadi Sh155. Kama wengine wanavyosema, wema hulipwa kwa wema, ninamuunga kwa uchaguzi ujao,” alisema. Hata hivyo, Seneta wa Murang’a, Joe Nyutu alimkosoa Rais, akisema ziara zake ni za kisiasa zaidi kuliko kushughulikia matatizo ya wananchi kama afya, barabara na usalama. Aliongeza kuwa utawala wake utapimwa kwa kigezo cha rushwa, madeni ya taifa na masuala ya haki za binadamu. Alisema pia kuwa Rais anaingia tena Mlima Kenya kwa “kampeni za udanganyifu” kuelekea 2027.
Original story
Continue reading at Taifa Leo (Swahili)
taifaleo.nation.co.ke
Summary generated from the RSS feed of Taifa Leo (Swahili). All article rights belong to the original publisher. Click through to read the full piece on taifaleo.nation.co.ke.
