“HUKU wapigakura wa eneobunge la Emurua Dikirr, Kaunti ya Narok wakielekea katika vituo vya kupigia kura leo kuchagua mbunge mpya, macho yataelekezwa katika pambano kali la kisiasa kati ya Rais William Ruto na aliyekuwa Naibu wake, Rigathi Gachagua. Uchaguzi huo mdogo umegeuka kuwa kipimo muhimu cha nguvu za kisiasa kati ya chama tawala cha United Democratic Alliance (UDA) na chama kipya cha Democracy for Citizens Party (DCP) kinachoongozwa na Bw Gachagua. Rais Ruto anataka chama chake kihifadhi kiti hicho kilichobaki wazi kufuatia kifo cha aliyekuwa mbunge Johana Ng’eno, huku Bw Gachagua akitarajia kupata ushindi wa kwanza wa chama chake katika Bunge la Kitaifa. Bw Ng’eno alifariki Februari 28, 2026 baada ya helikopta aliyokuwa akisafiria kuanguka katika eneo la Mosop, kaunti ya Nandi. Katika ajali hiyo, rubani George Were, mpiga picha Nick Kosgei, mwalimu Carlos Kibet Keter, askari wa Huduma ya Misitu Kenya (KFS) Amos Kipngetich Rotich na afisa wa itifaki wa serikali ya Narok Wycliff Kiprotich Rono pia walipoteza maisha. Masuala aliyokuwa akipigania marehemu sasa yamekuwa msingi wa kampeni za uchaguzi huo mdogo. Barabara mbovu, ukosefu wa hospitali bora, uhaba wa maji safi na miundombinu duni ni baadhi ya masuala yanayotawala kampeni huku serikali ikilaumiwa kwa kuwasahau wakazi baada ya uchaguzi mkuu. Wagombeaji watano wameidhinishwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kushiriki uchaguzi huo. Wanaopigiwa upatu ni David Kipsang Keter wa UDA na Vincent Rotich wa DCP. Wengine ni Desma Cherono wa PNU, Gideon Koech wa NVP na Keneth Kiprono wa RLP. Uchaguzi huo umeonekana kuwa wa hadhi ya juu kwa kuwa unafanyika miezi 16 kabla ya uchaguzi mkuu wa 2027, huku kila upande ukitaka kuonyesha kuwa una ushawishi mkubwa katika eneo la Bonde la Ufa ambalo lina kura nyingi. Wakili wa Nairobi Kipkirui Kemboi Kap Telwa alisema uchaguzi huo ni mtihani mkubwa kwa UDA. “Uchaguzi wa Emurua Dikirr utaonyesha iwapo Rais Ruto bado ana ushawishi katika Bonde la Ufa. Wakazi wa eneo hilo wamewahi kuasi viongozi walio mamlakani hapo awali,” alisema. Aliongeza kuwa tangu mwanzo, ilikuwa wazi kuwa Rais, Naibu wake Kithure Kindiki na mawaziri hawakukaribishwa kufanya kampeni eneo hilo kwa sababu wangemletea mgombea wa UDA madhara badala ya faida. Bw Gachagua pia alitarajiwa kufanya kampeni eneo hilo lakini akashauriwa asifanye hivyo kwa madai ya sababu za kiusalama. Rais Ruto, licha ya kuwa na makazi katika eneobunge jirani la Kilgoris, hajahudhuria hafla yoyote Emurua Dikirr tangu mazishi ya Bw Ng’eno Machi 6. Naibu Rais Profesa Kithure Kindiki pia hakufanya kampeni eneo hilo licha ya kuongoza kampeni za UDA katika maeneo mengine hapo awali. Katika hatua isiyo ya kawaida, viongozi wakuu wa UDA waliinua mikono na kuwaachia viongozi wa eneo hilo kuendesha kampeni. Gavana wa Narok Patrick Ntutu pia hakushiriki moja kwa moja kampeni hizo na badala yake alimtuma naibu wake Tamalinye Koech kuongoza shughuli za kampeni. Inasemekana Bw Ntutu hakuelewana kisiasa na Bw Keter na alikuwa amemuunga mkono Bennard Ngeno, aliyekuwa msaidizi wa marehemu Ng’eno, wakati wa kura za mchujo za UDA. Katika kura hizo za mchujo zilizofanyika Machi 27, Bw Keter alipata kura 13,749 dhidi ya kura 13,394 za Bw Ngeno. “Tumefanya kampeni kubwa za nyumba kwa nyumba na tuna imani tutashinda kiti hicho,” alisema Bw Tamalinye. Kwa upande mwingine, DCP ilipata nguvu baada ya ushindi katika uchaguzi mdogo wa wadi ya Narok Town mwaka jana ambapo mgombeaji wake alimshinda yule wa UDA.
Original story
Continue reading at Taifa Leo (Swahili)
taifaleo.nation.co.ke
Summary generated from the RSS feed of Taifa Leo (Swahili). All article rights belong to the original publisher. Click through to read the full piece on taifaleo.nation.co.ke.
