“Magonjwa ya mfumo wa kupumua kama kikohozi, mafua, maambukizi ya koo na nimonia ndiyo yanayoongoza kwa madai mengi ya matibabu yanayowasilishwa kwa Hazina ya Afya ya Jamii (SHA), kulingana na ripoti mpya ya malipo ya Bima ya Afya ya Jamii (SHIF). Ripoti hiyo ya kurasa 166 inaonyesha kuwa zaidi ya asilimia 21.4 ya madai yote yaliyoshughulikiwa na SHA kati ya Julai 2025 na Aprili 2026 yalihusiana na magonjwa ya mfumo wa kupumua. Hata hivyo, licha ya kuwa wagonjwa wake ni wengi, gharama ya matibabu yake ni ndogo ikilinganishwa na magonjwa mengine sugu. SHA, chini ya Mkurugenzi Mkuu Dkt Mercy Mwangangi, ilichukua nafasi ya NHIF kama mfumo mpya wa bima ya afya ya umma nchini. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, maambukizi ya mfumo wa juu wa kupumua kama mafua na kikohozi yalichangia zaidi ya asilimia 10 ya madai yote. Nimonia na mkamba (bronchitis) zilichukua asilimia 5.7 nyingine. Mkurugenzi mmoja wa SHA alisema magonjwa hayo hutibiwa kwa gharama ndogo kupitia ushauri wa daktari, dawa za kawaida na vipimo vya msingi. “Magonjwa yanayowajaza wengi hospitalini ndiyo rahisi zaidi kutibu kwa upande wa bima,” alisema. Ripoti ya Utafiti wa Uchumi ya KNBS pia ilionyesha kuwa magonjwa ya mfumo wa kupumua yaliongoza kwa visa vya maradhi nchini mwaka 2025 kwa visa milioni 15.4. Wizara ya Afya imeonya kuwa magonjwa hayo sasa ni tishio kubwa la afya ya umma huku magonjwa kama kifua kikuu, pumu na saratani ya mapafu yakiongezeka. Ripoti hiyo pia ilionyesha kuwa magonjwa ya tumbo kama vidonda vya tumbo yalichangia asilimia 17.8 ya madai yote ya SHA. Malaria nayo imeibuka kama janga kubwa baada ya visa kuongezeka kutoka milioni 3.8 mwaka 2024 hadi milioni 14.3 mwaka 2025. Ugonjwa huo ulichangia asilimia 9.8 ya madai yote na asilimia 6.7 ya matumizi ya SHA. Hata hivyo, magonjwa yanayotumia fedha nyingi zaidi ni saratani, magonjwa ya figo, moyo na huduma za uzazi. Saratani ilichangia asilimia 2.8 pekee ya madai lakini ikatumia asilimia 16.5 ya fedha zote za SHA kutokana na gharama ya matibabu, na uchunguzi maalumu. Magonjwa ya figo yalitumia asilimia 13.6 ya fedha zote huku wagonjwa wa kusafishwa damu wakihitaji matibabu ya mara kwa mara kila wiki. Huduma za uzazi zilichukua karibu asilimia 19 ya matumizi yote ya SHA huku upasuaji wa kujifungua ukiongezeka nchini. Ajali za barabarani pia zimeendelea kutumia fedha nyingi kutokana na gharama ya upasuaji, ICU na matibabu ya muda mrefu.
Original story
Continue reading at Taifa Leo (Swahili)
taifaleo.nation.co.ke
Summary generated from the RSS feed of Taifa Leo (Swahili). All article rights belong to the original publisher. Click through to read the full piece on taifaleo.nation.co.ke.
