skipToContent
🌐Secondary

Shule zinavyokumbatia mapishi safi kuokoa mazingira na gharama

Shule zinavyokumbatia mapishi safi kuokoa mazingira na gharama
KWA muda mrefu, shule nyingi nchini Kenya zimekuwa zikitegemea kuni kuandaa chakula cha wanafunzi mfumo ambao hata ingawa ni maarufu umeendelea kuwa mzigo mkubwa kwa sababu ya gharama zake, changamoto za kiafya na uharibifu wa mazingira. Majiko mengi ya shule, moshi mzito ulikuwa sehemu ya maisha ya kila siku. Wapishi walilazimika kufanya kazi kwa saa nyingi katika mazingira yenye hewa chafu huku wanafunzi wakichelewa kupata chakula, hasa wakati wa mvua ambapo kuni huwa mbichi na vigumu kuwaka. Katika maeneo kame na nusu-kame (ASAL), changamoto hiyo imekuwa kubwa zaidi. Mahitaji ya kuni yameongeza ukataji miti, hali inayochochea athari za mabadiliko ya tabianchi kama vile ukame wa muda mrefu, mvua zisizotabirika na upungufu wa malisho kwa mifugo. Hata hivyo, hali hiyo inaanza kubadilika huku baadhi ya shule zikikumbatia matumizi ya majiko ya kisasa yanayotumia umeme na nishati ya jua (solar). Teknolojia hiyo mpya haipunguzi gharama za utendakazi, bali pia inalinda mazingira na kuboresha huduma ya lishe shuleni. Katika Shule ya Al-Huda Muslim iliyoko eneo la Majengo, Kaunti ya Kajiado, matumizi ya kuni yalikuwa yamekuwa changamoto kubwa kwa taasisi hiyo ya elimu hiyo yenye zaidi ya wanafunzi 820. Kwa mwezi, ilikuwa ikinunua magari mawili ya kuni kwa gharama ya karibu Sh20,000 kila mwezi, mbali na gharama nyingine za maji na shughuli za jikoni. Kwa jumla, zaidi ya Sh40,000 zilikuwa zikitumika kila mwezi kuendesha mpango wa chakula. [caption id="attachment_187993" align="aligncenter" width="300"] Joy Kwamboka kutoka EcoBora akielezea kuhusu majiko ya umeme na nishati ya jua. Picha|Sammy Waweru [/caption] Mwalimu anayesimamia mazingira na mpango wa lishe shuleni humo, Shaaban Iddi, anasema changamoto ya kuni ilikuwa kubwa zaidi ikikunbukwa kuwa Kajiado ni eneo lenye uhaba wa miti. “Wakati mwingine tulilazimika kuomba ruhusa kutoka kwa serikali ya kaunti kukata miti ili kuongeza kuni, jambo ambalo lilisababisha kuchelewa kwa maandalizi ya chakula,” anakumbuka. Mbali na gharama hizo, moshi kutoka jikoni uliathiri afya ya wafanyakazi. “Wapishi walifanya kazi kwa muda mrefu katika mazingira yenye moshi mwingi uliowaathiri kiafya,” Mwalimu Shaaban anaeleza. Lakini baada ya shule hiyo kuanza kutumia majiko yanayotumia umeme na nishati ya jua yaliyotengenezwa na kampuni ya EcoBora, hali ilianza kubadilika. Kwa sasa, chakula huiva kwa haraka, mazingira ya jikoni ni safi zaidi na wanafunzi hupata chakula kwa wakati unaofaa. “Masomo yanaendelea bila usumbufu kwa sababu chakula kinapatikana kwa wakati,” Shaaban anasema. Pia, anasema shule hiyo imeongeza juhudi za uhifadhi wa mazingira kwa kuhimiza upandaji miti hasa ya matunda kama vile maparachichi na karakara. “Klabu ya mazingira huwapa wanafunzi motisha ya kupanda na kutunza miti hadi wanapomaliza masomo yao,” anaongeza. Katika Kaunti ya Kiambu, PCEA Mama Ngina Primary and Junior Secondary School pia imeanza kutumia mfumo wa mapishi safi. Shule hiyo yenye karibu wanafunzi 2,500 ilikuwa ikikumbwa na changamoto ya moshi kutoka jikoni kutokana na madarasa mengi kuwa karibu na eneo la kupikia. Naibu mwalimu mkuu anayesimamia utawala, Rachael Ndune, anasema matumizi ya kuni yalikuwa yakichangia matatizo ya kiafya miongoni mwa wapishi. “Wafanyakazi wengi walikuwa wakiugua mara kwa mara kutokana na moshi na wakati mwingine walishindwa kufika kazini,” anasema. [caption id="attachment_187994" align="aligncenter" width="300"] Naibu mwalimu mkuu anayesimamia utawala, PCEA Mama Ngina Primary and Junior Secondary School, Kaunti ya Kiambu Rachael Ndune. Picha|Sammy Waweru [/caption] Kulingana na Ndune, shule hiyo ilikuwa ikitumia karibu Sh300,000 kwa muhula kununua kuni, huku zile mbichi zikisababisha chakula kuchukua muda mrefu kuiva. Kupitia matumizi ya majiko ya kisasa ya EcoBora, shule hiyo sasa inapunguza matumizi ya kuni na kuokoa muda wa maandalizi ya chakula. EcoBora ni kampuni yenye makao yake Nairobi na kiwanda cha kutengeneza majiko ya umeme na nishati ya jua katika Kaunti ya Kajiado. Mkufunzi wa wapishi kutoka EcoBora, Yvonne Nyambura, anasema taasisi zinazonunua majiko hayo hupatiwa mafunzo ya siku tatu hadi saba kuhusu matumizi bora ya nishati, usalama na utengenezaji vifaa. “Chakula kama githeri ambacho hapo awali kilikuwa kikichukua saa tano au sita kuiva kwa kutumia kuni, sasa huiva ndani ya saa mbili au tatu,” anasema. Kulingana na Joy Kwamboka kutoka EcoBora, Kenya ina zaidi ya taasisi 92,000 za elimu, zikiwemo shule na vyuo, na matumizi ya majiko safi yanaweza kuwa suluhisho muhimu katika kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi. Anasema shule moja inaweza kutoa hadi tani 700 za hewa ya kaboni kutokana na matumizi ya kuni. “Shule zikihamia matumizi ya umeme na nishati ya jua, zitapunguza ukataji miti, kupunguza uzalishaji wa hewa chafu na kuelekeza fedha zilizookolewa katika kuboresha lishe ya wanafunzi au miradi mingine ya maendeleo,” anaelezea. Kampuni hiyo hutengeneza majiko ya lita 20 hadi 2,000 kulingana na mahitaji ya wateja. Kadri Kenya inavyoendelea kushuhudia athari za mabadiliko ya tabianchi, shule zinaibuka kama sehemu muhimu katika juhudi za kulinda mazingira. Kupitia matumizi ya mapishi safi, taasisi za elimu zinaonyesha kuwa vita dhidi ya mabadiliko ya tabianchi vinaweza kuanzia shuleni huku watoto wakijifunza umuhimu wa kuhifadhi mazingira kwa kizazi cha sasa na kijacho.
Share
Original story
Continue reading at Taifa Leo (Swahili)
taifaleo.nation.co.ke
Read full article

Summary generated from the RSS feed of Taifa Leo (Swahili). All article rights belong to the original publisher. Click through to read the full piece on taifaleo.nation.co.ke.