“Katika jamii ya sasa ya mitandao ya kijamii, ambapo wanawake hupokea maelfu ya ujumbe kila siku, umakini umekuwa bidhaa ya thamani kubwa. Ndiyo maana mwanaume wa thamani ya juu hampi mwanamke umakini bure. Hatoi muda wake kwa urahisi bila kusudi au malengo. Anaweza kumkaribia mwanamke na kujitambulisha ili kuanzisha mawasiliano, lakini baada ya hapo, anajua kusimama kidete na kuendelea na maisha yake bila kumfanya awe kitovu cha kila kitu. Hii humweka katika nafasi ya heshima na kuvutia kwa sababu haonekani kuwa mtu wa kutegemea hisia. Kipengele kingine muhimu ni kuwa na malengo makubwa maishani. Mwanaume wa thamani ya juu huwa na dira yake, anajua anachotaka na anajituma kukifikia. Hana muda wa kupoteza kwenye mahusiano yasiyo na maana au “flirting” isiyo na tija. Badala yake, nguvu zake huwekeza kujenga maisha yenye mafanikio, kazi, biashara au maendeleo binafsi. Hali hii ya kujituma na kuwa na mwelekeo huonekana kuvutia wanawake kwa sababu inaonyesha uthabiti na uwezo wa kuongoza maisha yake bila kuyumbishwa. Ujasiri pia ni sifa muhimu. Mwanaume wa aina hii haogopi kuchukua hatua. Anapotaka kitu, anaenda moja kwa moja bila kuchelewesha. Kuchelewa au kusubiri “bahati” ni tabia ya watu wasiojiamini. Anajua kwamba kufanikiwa maishani kunahitaji hatari ndogo na maamuzi ya haraka. Hivyo, hata katika mahusiano, haogopi kumkaribia mwanamke au kuonyesha hisia zake kwa uwazi bila kukubali zimfanye mtumwa. Pia, mwanaume wa thamani ya juu haogopi kuwa peke yake. Anaelewa kuwa thamani yake haitegemei kuwa katika uhusiano. Wanaume wengi huingia na kutoka katika mahusiano kwa sababu wanaogopa upweke, lakini yeye anaona upweke kama muda wa kujijenga. Hii humpa nguvu ya kipekee na kujiamini, ambayo mara nyingi huwavutia wanawake zaidi kuliko kuonekana mwenye uhitaji. Aidha, anaepuka kushiriki katika migogoro isiyo na maana. Ikiwa mwanamke ana tabia ya kuanzisha ugomvi usio wa msingi au hisia zisizo na mantiki, hataki kujihusisha nazo. Anajua thamani ya amani na heshima katika mahusiano. Kutojibu kila mzozo humfanya aonekane mtu mwenye udhibiti wa hisia zake na mwenye msimamo. Mwanaume wa aina hii pia huwa mkweli. Hapotezi muda kucheza michezo ya akili au kupoteza muda wa wengine. Ikiwa mambo hayaendi sawa, anaweza kuondoka au kupunguza mawasiliano bila drama. Hii humfanya mwanamke kuelewa kuwa muda na nafasi yake ni za thamani na hazipatikani kirahisi. Mwanamume anayejua thamani yake, hatabadilisha mipango yake kwa ajili ya kila mtu. Ana ratiba yake na anaithamini. Hata akikutana na mwanamke anayemvutia, haachi majukumu yake muhimu. Hii inaonyesha kuwa ana maisha yake binafsi na haishi kwa ajili ya kumfurahisha mtu mmoja tu. Hali hii huongeza heshima kwake na kumfanya aonekane mtu mwenye msimamo. Hatimaye, mawazo yake ndiyo msingi wa kila kitu. Anaamini katika thamani yake binafsi na haoni wanawake kama viumbe wa ajabu wanaomzidi. Hii humfanya awe na utulivu na kujiamini akiwa nao. Badala ya woga au wasiwasi, anaingia katika mazungumzo kwa utulivu na uhalisia, jambo ambalo mara nyingi huvutia zaidi kuliko kujifanya au kuogopa kukataliwa. Mwanaume wa thamani ya juu si tu kuhusu mahusiano, bali ni kuhusu nidhamu, malengo na mtazamo wa maisha. Ni mtu anayejijenga kwanza kabla ya kutafuta kuthibitishwa na wengine.
Original story
Continue reading at Taifa Leo (Swahili)
taifaleo.nation.co.ke
Summary generated from the RSS feed of Taifa Leo (Swahili). All article rights belong to the original publisher. Click through to read the full piece on taifaleo.nation.co.ke.
