“JOPO la kuamua Migogoro ya Vyama vya Kisiasa limezima utekelezaji wa matokeo yoyote yatakayotokana na mchakato wa kinidhamu wa chama cha ODM unaolenga kumtimua Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna kama katibu mkuu, hadi kesi aliyowasilisha itakaposikilizwa na kuamuliwa. Hata hivyo, jopo hilo halikusimamisha mchakato wa ndani wa chama wa kusuluhisha migogoro (IDRM), likieleza kuwa unaweza kuendelea lakini maamuzi yoyote yatakayofikiwa hayatatiliwa maanani hadi kesi hiyo iamuliwe kikamilifu. “Tunabaini kuwa ni muhimu kutoa maagizo ya kulinda mamlaka ya jopo hili. Hatusimamishi mchakato wa IDRM au kesi zozote kati ya mlalamishi na mshtakiwa wa kwanza (ODM),” lilisema jopo hilo. “Hata hivyo, tunaagiza kuwa matokeo ya mchakato wowote huo hayataanza kutekelezwa hadi kesi hii isikilizwe na kuamuliwa,” ikaongeza. Maagizo hayo yanamaanisha kuwa ODM inaweza kuendelea na mchakato wake wa kinidhamu, lakini haiwezi kutekeleza uamuzi wowote dhidi ya Seneta Sifuna hadi mgogoro huo utakapotatuliwa na jopo hilo la mahakama. Kesi hiyo ilitokana na azimio la Kamati Kuu ya Kitaifa (NEC) ya ODM la Februari 11, lililopendekeza kuondolewa kwa Seneta Sifuna katika wadhifa wake kwa madai ya utovu wa nidhamu. Chama hicho kilimshutumu kwa kupinga misimamo rasmi ya ODM, kukosa kuhudhuria mikutano muhimu na kushiriki shughuli za kisiasa zisizoidhinishwa, ukiwemo mpango wa Linda Mwananchi. Hata hivyo, Bw Sifuna anapinga madai hayo na kudai kuwa mchakato uliotumika kumuondoa haukuwa halali na ulikiuka haki yake ya kusikilizwa kwa haki. Aliwasilisha malalamishi katika jopo akitaka kusitishwa kwa azimio la NEC pamoja na hatua zozote za kinidhamu dhidi yake. Pia, aliomba chama kizuiwe kuchapisha kuondolewa kwake kwenye Gazeti Rasmi la Serikali na Msajili wa Vyama vya Kisiasa hadi kesi hiyo itakapoamuliwa. Kwa upande wake, ODM ilipinga maombi hayo ikisisitiza kuwa mgogoro huo unapaswa kushughulikiwa kupitia mifumo ya ndani ya chama, ikidai kuwa jopo hilo halina mamlaka katika hatua ya sasa. Chama kilieleza kuwa azimio la NEC halikuwa uamuzi wa mwisho bali lilianzisha tu mchakato wa kinidhamu, na hivyo mahakama inapaswa kuruhusu taratibu zake ziendelee. Hata hivyo, jopo la mahakama lililoongozwa na mwenyekiti Gad Gathu lilikataa pingamizi la awali la ODM kuhusu mamlaka yake. Jopo lilibaini kuwa suala la iwapo Bw Sifuna alifuata ipasavyo taratibu za ndani za chama haliwezi kuamuliwa bila ushahidi. “Hoja zilizotolewa zinahitaji uchambuzi wa ukweli na ushahidi, na hivyo haziwezi kushughulikiwa kupitia pingamizi la awali,” lilisema jopo hilo. Jopo hilo pia lilibaini kuwa Bw Sifuna aliandikia chama Aprili 1 akitaka mgogoro utatuliwe ndani ya chama, lakini ODM ilikataa. Kuhusu ombi la amri za muda, jopo lilisema haikuhitajika kutoa uamuzi wa mwisho katika hatua hiyo, bali kubaini iwapo mlalamishi ameonyesha hoja ya msingi inayostahili kusikilizwa. Aidha, lilikubaliana kuwa hoja zilizowasilishwa, ikiwemo madai ya kukiukwa kwa haki na uhalali wa mchakato wa kinidhamu, zinahitaji kujibiwa na ODM. “Swali la iwapo haki za mlalamishi zilikiukwa linahitaji majibu kutoka kwa mshtakiwa,” ilisema. Katika kulinda kesi hiyo, jopo pia lilizingatia hatari ya kesi kupoteza maana ikiwa hatua za muda hazingechukuliwa. Lilibainisha kuwa hali hiyo haimaanishi tu kuwa kesi itakuwa bure, bali pia inaweza kudhoofisha ufanisi wa mchakato wa kisheria. Kesi hiyo itatajwa tena Juni 9 saa nane na nusu mchana. Mgogoro huu unaashiria vita mpya ya kisheria kati ya Bw Sifuna na ODM, baada ya kesi ya awali kutupiliwa mbali kwa kukosa kukamilisha taratibu za ndani za chama. Baada ya uamuzi huo, Bw Sifuna aliwasiliana na chama akitaka suluhu, lakini ODM ilikataa na kumwelekeza kwa mchakato wa kinidhamu. Kwa mujibu wa katiba ya ODM, kamati ya nidhamu ina mamlaka ya kusikiliza kesi na kupendekeza adhabu kuanzia onyo hadi kufukuzwa uanachama, kulingana na idhini ya vyombo vya juu vya chama.
Original story
Continue reading at Taifa Leo (Swahili)
taifaleo.nation.co.ke
Summary generated from the RSS feed of Taifa Leo (Swahili). All article rights belong to the original publisher. Click through to read the full piece on taifaleo.nation.co.ke.
