“WAGOMBEAJI wanaosaka kuungwa na wapigakura 44,447 katika uchaguzi mdogo wa eneobunge la Emurua Dikirr, Kaunti ya Narok, wamesalia na leo pekee kufanya kampeni. Uchaguzi huo mdogo utaandaliwa Alhamisi ambapo mrithi wa mbunge wa eneo hilo Johana Ng’eno atapatikana. Ushindani unaonekana kuwa kati ya chama cha UDA cha Rais William Ruto, kinachotaka kuhifadhi kiti hicho, na DCP ya aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua. Tume ya Uchaguzi (IEBC) imesema maandalizi yote yamekamilika kwa uchaguzi huo. Bw Ng’eno, alifariki katika ajali ya helikopta eneo la Mosop, Kaunti ya Nandi, mnamo Februari 28, 2026. David Kipsang Keter ndiye mgombea wa UDA, huku Vincent Kibet Rotich akipeperusha bendera ya DCP. Wawili hao wanatazamwa kuwa wagombea wakuu wa kiti hicho katika eneo ambalo wapigakura na viongozi huwa hawafuati umaarufu wa chama bali utendakazi wa kiongozi. Wawaniaji wengine ni Gideon Koech, wakili kutoka Bomet, wa NVP na mfanyabiashara Desma Cherono wa PNU. Wawili hao wameendesha kampeni za chini kwa chini ikilinganishwa na Mabw Keter na Rotich. Wagombea hao wamekuwa wakizunguka wadi nne za Mogondo, Kapsasian, Ilkerin na Ololmasani wakisaka kura za vijana na wanawake katika eneo ambalo wakazi wake wanasema limekuwa nyuma kimaendeleo chini ya serikali ya sasa na zilizopita. Ukosefu wa miundombinu bora, hasa barabara na madaraja, pamoja na uhaba wa vituo vya afya na miradi ya maji, yamekuwa masuala makuu yaliyotawala kampeni katika kipindi cha miezi miwili iliyopita. Bw Keter, ambaye amewahi kushindwa mara tatu na marehemu Bw Ng’eno, amewataka wanawake na vijana kumuunga mkono akiahidi kushirikiana na serikali kuhakikisha miradi iliyoanzishwa na mbunge huyo wa zamani inakamilika. “Kwa miezi michache iliyosalia kabla ya uchaguzi mkuu ujao, nikichaguliwa nitafanya kazi kwa karibu na serikali kuharakisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo iliyoanzishwa na mbunge wetu marehemu,” alisema akasema Bw Keter. Kwa upande wake, Bw Rotich, aliwahi kuhudumu kama Mwakilishi wa Wadi ya Mogondo, alisema wakazi wa eneo hilo wamechoshwa na ahadi zisizotekelezwa. “Haitakuwa mara ya kwanza kwa wakazi wa Emurua Dikirr kwenda kinyume na matarajio ya wengi. Ikumbukwe kwamba uchaguzi mkuu uliopita ndio mara ya kwanza marehemu mbunge wetu alichaguliwa kupitia chama maarufu. Kabla ya hapo alikuwa akishinda kupitia vyama vidogo vilivyopuuzwa,” akasema Bw Rotich.
Original story
Continue reading at Taifa Leo (Swahili)
taifaleo.nation.co.ke
Summary generated from the RSS feed of Taifa Leo (Swahili). All article rights belong to the original publisher. Click through to read the full piece on taifaleo.nation.co.ke.
