skipToContent
🌐All

TAHARIRI: Makongamano yatakuwa na tija iwapo raia atafaidi

TAHARIRI: Makongamano yatakuwa na tija iwapo raia atafaidi
HII leo ni siku ya pili na ya mwisho ya Kongamano kati ya Ufaransa na Mataifa ya Afrika linalofanyika jijini Nairobi, Kenya. Kongamano hili limewaleta pamoja viongozi wa kisiasa, wawekezaji, wataalamu wa uchumi na wadau mbalimbali kujadili mustakabali wa ushirikiano kati ya Afrika na Ufaransa. Rais William Ruto wa Kenya pamoja na Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa ndio wenyeji wa mkutano huo wenye umuhimu mkubwa kwa bara la Afrika. Ajenda zilizowekwa mezani ni pamoja na uwekezaji katika viwanda visivyochafua mazingira, mageuzi ya mfumo wa utoaji mikopo duniani, amani na usalama, uchumi wa shughuli za majini, kilimo na utoshelevu wa chakula, pamoja na matumizi ya akiliunde na mageuzi ya kidijitali. Hakuna shaka kuwa masuala haya ni muhimu kwa maendeleo ya mataifa ya Afrika ambayo bado yanakabiliwa na changamoto nyingi za kiuchumi na kijamii. Hata hivyo, swali kubwa ambalo wananchi wengi wanajiuliza ni iwapo kongamano hili litazaa matunda yatakayogusa maisha yao ya kila siku. Historia imeonyesha kuwa makongamano mengi ya kimataifa hujaa hotuba nzuri, ahadi tamu na maazimio makubwa, lakini utekelezaji wake hubaki kuwa wa kusuasua au kutotekelezwa kabisa. Mwananchi wa kawaida hahitaji kusikia maneno matupu bali anahitaji kuona mabadiliko halisi katika maisha yake. Kwa mfano, ikiwa viongozi wanajadili kilimo na usalama wa chakula, basi wakulima wanapaswa kupata mbegu bora, masoko ya uhakika na pembejeo kwa bei nafuu. Ikiwa wanajadili uchumi wa kidijitali na akiliunde, vijana wanapaswa kupata ajira, mafunzo ya teknolojia na mazingira bora ya ubunifu. Vivyo hivyo, mazungumzo kuhusu mageuzi ya mfumo wa utoaji mikopo duniani yanapaswa kusaidia mataifa ya Afrika kupata mikopo yenye masharti nafuu ili fedha hizo zitumike kuboresha huduma za afya, elimu na miundombinu. Aidha, viongozi wa Afrika wanapaswa kuhakikisha kuwa ushirikiano wa kimataifa hauwi njia ya mataifa makubwa kunufaika pekee huku Afrika ikiendelea kubaki katika umaskini. Ni lazima kuwepo uwazi, uwajibikaji na usimamizi bora wa miradi itakayozaliwa kutokana na kongamano hili. Kwa hakika, mafanikio ya kongamano hili hayatapimwa kwa ukubwa wa hotuba wala idadi ya viongozi waliohudhuria, bali kwa namna litakavyobadilisha maisha ya wananchi wa kawaida. Wananchi wanahitaji kuona ajira zikiongezeka, gharama ya maisha ikipungua, chakula kikipatikana kwa urahisi na mazingira ya biashara yakiimarika. Hapo ndipo kongamano hili litakuwa na maana ya kweli kwa Waafrika.
Share
Original story
Continue reading at Taifa Leo (Swahili)
taifaleo.nation.co.ke
Read full article

Summary generated from the RSS feed of Taifa Leo (Swahili). All article rights belong to the original publisher. Click through to read the full piece on taifaleo.nation.co.ke.