“KWA kawaida wakulima wengi nchini wamekuwa wakitumia gharama nyingi kuzalisha chakula. Aidha wamekuwa wakiwekeza hela nyingi katika dawa za wadudu husika ili kulinda mazao yao dhidi ya wadudu hatari au mkurupuko wa aina mbalimbali ya magonjwa. Changamoto nyingine ambayo inawalemea ni namna ya kupata soko kwa mazao yao ghafi hasa wakati ambapo bidhaa huwa zimefurika sokoni. Hata hivyo, jambo linalowafanya wengi wao kupoteza maelfu ya pesa ni uhaba wa miundo misingi faafu kama vile majokofu ya kisasa aina ya ‘cold rooms’ ambayo husaidia kutunza mazao kwa muda mrefu. Pia, kero la mabroka si jambo geni na limekuwa donda sugu. Kwa muda mrefu wamekuwa wakinunua mazao kutoka shambani kwa bei ya chini na kisha kuyauza sokoni kwa bei ya juu, jambo linalowafanya wakulima wadogo vijijini waendelee kutumbukia kwenye lindi la umaskini. Tom Obote kijana ambaye amewekeza katika kilimo cha aina mbalimbali ya mazao, anasema kwa kutumia teknolojia, masaibu ya wakulima yatapungua kwa asilimia 50. Kwenye mahojiano na Akilimali , alisema kuwa wakulima wengi wameweka matumaini yao yote kwa mabroka kwa sababu hawajui wapeleke mazao yao wapi muda baada ya kukomaa. Anasema njia mojawapo ya kukabiliana na kero za mabroka ni kukumbata teknolojia za kisasa ambazo kwa njia moja huwaunganisha wakulima na soko. Kwa mfano matumizi ya apu za simu ambazo huwakutanisha wanunuzi na wauzaji chakula. Anasema kanuni za kilimo bora ni uwezo wa kufuata miongozo wa Kisayansi iliyofanyiwa majaribio kwa muda mrefu ambapo vilevile mkulima anaweza kujifunza baadhi ya taratibu hizi na akazifanyia kazi akiwa nyumbani. Mbali na kuwaunganisha na wanunuzi, pia huwasaidia kutangamana na wataalamu wa kilimo waliokita katika nyanja tofauti kutoa ushauri wa kitaalamu. Apu hizo pia hutoa mafunzo ya kisasa kuhusu mbinu bora za ukulima kwa ajili ya kulenga zaidi soko la kimataifa. “Hapa wanaweza kuzingatia mahitaji ya kimsingi kwenye soko la kimataifa na pia kuzingatia afya ya jamii," asema. Pili, anasema mazao mengi yanapofikishwa sokoni hukosa kupimwa kwenye ratili. Anasema hatua ya upimaji kwa kutumia ratili ni muhimu kwa sababu humsaidia mkulima kufanya maamuzi sahihi kama kubaini faida ya kilimo chake. Pia mkulima anaweza kudumisha usalama wa chakula kwa sababu anaweza kutenganisha vitu visivyohitajika ambavyo huenda vimechanganyika na chakula. "Udhibiti wa ubora wa chakula husaidia wanunuzi kuepuka mseto wa chakula na aina nyingine ya vitu kama vile mawe ambavyo havihitajiki," Anasema mkulima yeyote ambaye anaendesha kilimo biashara anatakiwa kujipimia bidhaa zake kabla hazijaingia sokoni. Anaongeza kuwa sehemu kubwa ya wakulima hawajakuwa wakipata ushauri wa kitaalam, pembejeo bora na vitabu vya kilimo bora vilivyosheheni mbinu za kisasa na miongozo sahihi itakayowawezesha kuboresha kilimo na kuongeza mazao mara dufu. Kadhalika, anasema changamoto nyingine iliyopo kwenye utekelezaji wa baadhi ya mageuzi muhimu ni uwezo dhaifu wa utekelezaji wa sheria za kukabiliana na mabroka.
Original story
Continue reading at Taifa Leo (Swahili)
taifaleo.nation.co.ke
Summary generated from the RSS feed of Taifa Leo (Swahili). All article rights belong to the original publisher. Click through to read the full piece on taifaleo.nation.co.ke.
