skipToContent
🌐All

Ubabe: Linda Mwananchi yawika Linda Ground ikififia

Ubabe: Linda Mwananchi yawika Linda Ground ikififia
VUGUVUGU la Linda Mwananchi limeanza kuwika tena huku Linda Ground ikionekana kufifia, taswira inayodhihirisha mabadiliko mapya ya kisiasa yanayozidi kuchipuka kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027. Leo vuguvugu hilo linaloongozwa na Katibu Mkuu wa ODM na Seneta wa Nairobi, Edwin Sifuna, litafanya mkutano mkubwa Machakos katika kile kinachoonekana kama juhudi za kuimarisha ushawishi wake mashinani huku miungano mipya ikiendelea kusukwa. Katika ujumbe aliochapisha kwenye ukurasa wake wa mtandao wa X mnamo Ijumaa, Mei 29, 2026, Mbunge wa Suba Kusini Caroli Omondi alitoa ujumbe mfupi lakini uliosisimua wafuasi wa vuguvugu. “Tumerejea! Tupatane Machakos Jumapili Mei 31, 2026,” aliandika. Wachanganuzi wametafsiri tangazo hilo kama ishara ya kuongezeka kwa shughuli za kundi la Linda Mwananchi ambalo linaendelea kujipanga upya baada ya ODM kuachana rasmi na kaulimbiu ya “Linda Ground”. Machakos ambako mkutano huo utafanyika ni mojawapo ya ngome kuu za kisiasa za kiongozi wa Wiper, Kalonzo Musyoka, na eneo muhimu kwa muungano wa upinzani ambao unalenga kusuka ushirikiano na vuguvugu la Seneta Sifuna. Hatua hiyo inaonekana kuongeza uzito wa kisiasa wa mkutano huo huku vinara wa upinzani wakisaka njia mpya za kuunganisha nguvu dhidi ya utawala wa Rais William Ruto. Mkutano huo unatarajiwa kuvutia viongozi na wafuasi kutoka maeneo mbalimbali huku kampeni zikianza kushika kasi kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027. Tangazo la Omondi limejiri siku chache baada ya Gavana wa Homa Bay Gladys Wanga kufichua kuwa ODM imeachana na kaulimbiu ya “Linda Ground” baada ya madai kwamba baadhi ya makundi yalikuwa yameanza kuipotosha kisiasa. Akizungumza katika mkutano wa mashauriano na wawaniaji wanaosaka tikiti ya ODM, mjini Kisumu mnamo Jumatatu, Gavana Wanga alisema wanachungwa sasa wanapaswa kutumia nembo na rangi rasmi za chama hicho pekee. “Tulikuwa tumeanzisha vuguvugu la Linda Ground ili kuimarisha msingi wetu wa kisiasa, lakini baadhi ya watu walikuja na mambo tofauti. Sasa tumeachana na hilo. Sisi ni ODM na rangi yetu ni chungwa,” alisema Wanga. Aidha, alisisitiza kuwa ODM bado imeungana chini ya uongozi wa Seneta wa Siaya Oburu Oginga licha ya pandashuka zinazoendelea ndani ya chama hicho cha chungwa. Ingawa ajenda rasmi ya mkutano wa Machakos bado haijawekwa wazi, mkutano huo tayari umechochea mjadala kuhusu uwezekano wa kuundwa kwa ushirikiano mpya wa kisiasa kati ya vinara wa upinzani na kundi la Linda Mwananchi. Kurejea kwa mikutano ya kisiasa mashinani na kuibuka kwa mirengo mipya kunaonyesha jinsi ushindani wa kisiasa unazidi kushika kasi nchini huku viongozi wakijipanga kwa kura ya mwaka ujao. Wakati huo huo, Gavana wa Siaya James Orengo ameapa kuwa vuguvugu la Linda Mwananchi halitatishwa baada ya mmoja wa wafuasi wake Evans “Kidero Jasuba” Kawala kukamatwa na baadaye kuachiliwa kwa dhamana. Katika taarifa yake ya Mei 28, 2026, Bw Orengo alisema timu ya mawakili iliyoongozwa na Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino ilisaidia kuachiliwa kwa Kawala huku akisisitiza kuwa wanachama wa vuguvugu hilo waliendelea kuonyesha mshikamano. “Kama Linda Mwananchi, hatutakubali kurudi nyuma. Tulisimama bega kwa bega na Evans ‘Kidero Jasuba’ Kawala kufuatia kukamatwa kwake kwa misingi ya kisiasa,” alisema Bw Orengo. Pia aliwasifu wanachama wa mtandao wa Bunge la Wananchi kwa kujitokeza kwa wingi mahakamani kama ishara ya mshikamano. “Heshima kubwa kwa familia ya Bunge la Wananchi kwa kujitokeza na kusimama imara kwa mwenzao,” alisema. Awali, Bw Orengo alikuwa ameishutumu serikali kwa madai ya kumteka nyara Kawala kwa sababu ya kuikosoa serikali ya Rais Ruto. Kwa upande wake, DCI ilisema Kawala alikamatwa kutokana na matamshi ya uchochezi yaliyokuwa yakisambazwa kwenye mitandao ya kijamii. Katika taarifa yake ya Mei 27, 2026, DCI ilisema maudhui hayo yalionekana kuhatarisha mshikamano wa kitaifa pamoja na utulivu wa nchi.
Share
Original story
Continue reading at Taifa Leo (Swahili)
taifaleo.nation.co.ke
Read full article

Summary generated from the RSS feed of Taifa Leo (Swahili). All article rights belong to the original publisher. Click through to read the full piece on taifaleo.nation.co.ke.