“WAKAZI wa Lamu pamoja na wanaharakati wa haki za binadamu wameitaka serikali kutekeleza amri ya mahakama iliyosimamisha marufuku ya safari za usiku katika kaunti hiyo, ambayo imekuwa ikitekelezwa kwa miaka tisa. Mahakama Kuu ya Garsen, Kaunti ya Tana River, ilisitisha utekelezaji wa amri hiyo Alhamisi iliyopita, ikitoa afueni kubwa kwa wakazi. Jumanne, mabasi, malori na magari mengine yanayopita katika barabara ya Lamu-Witu-Garsen yalifunga makutano ya barabara Minjila, huku madereva wakipinga vizuizi vya kusafiri saa kumi na mbili jioni hadi saa moja asubuhi. Hali hiyo ililazimisha magari na abiria wanaotoka pande zote za Lamu, Garsen, Garissa, Malindi na Mombasa kusimama kwani hakukuwa na njia ya kupita kuendelea na safari zao. Bw Mohamed Skanda, mwanaharakati, alisema kukaidi amri halali ya Mahakama Kuu ni kudharau mahakama na matumizi mabaya ya mamlaka. Kufikia saa sita mchana, mamia ya abiria bado walikuwa wamekwama Minjila huku magari yakiendelea kufunga barabara na hakuna gari lililoruhusiwa kupita upande wowote. Amri ya mahakama ilifuata ombi lililowasilishwa na wakazi 24 na wanaharakati waliodai kuwa, marufuku ya kusafiri usiku iliyowekwa mwaka wa 2017 ilifaa idumu kwa siku 90 pekee na haikuwahi kuongezwa kisheria. Kulingana nao, ingawa kafyu ilikuwa na msingi kutokana na mashambulio ya kigaidi yaliyokuwa yakishuhudiwa, ilipoteza uhalali wake kisheria Oktoba 2017 baada ya muda wa siku 90 uliotolewa chini ya Tangazo la Kisheria Na. 107 la 2017 kumalizika. “Hakujawahi kutolewa tangazo jipya la serikali kuongeza au kurejesha marufuku hiyo, hivyo utekelezaji wake ni haramu,” walieleza katika nyaraka za mahakama. Miongoni mwa waliowasilisha kesi hiyo ni mwenyekiti wa Usimamizi wa Ufukwe Bubakar Mohamed Twalib, mlezi wa jamii ya Bajuni Omar Shariff Ali, mwanaharakati Hussein Khalid na viongozi wa Muslims for Human Rights. Walalamishi walishtaki Wizara ya Usalama wa Ndani, Inspekta Jenerali wa Polisi, Huduma ya Kitaifa ya Polisi na Mwanasheria Mkuu wakitaka marufuku hiyo isimamishwe mara moja hadi kesi itakaposikizwa na kuamuliwa. Jana, wakazi walisema vizuizi hivyo vya muda mrefu vimevuruga sana uchumi wa eneo hilo, hasa uvuvi, biashara na utalii ambazo hutegemea sana shughuli za usiku na usafiri. Pia walisema vimeathiri upatikanaji wa huduma za dharura za afya na kuingilia taratibu za mazishi ya Kiislamu zinazohitaji maziko ya haraka. “Tutaendelea kufunga barabara hadi polisi watuhakikishie kuwa safari za usiku zimeruhusiwa tena. Tumechoshwa na usumbufu huu kutoka kwa vyombo vya usalama. Kwa nini wanatuzuia kusafiri usiku?” alisema dereva Mohamed Omar. Katika baadhi ya maeneo ya Minjila Junction, wasafiri waliweka vizuizi barabarani na kuchoma magurudumu hali iliyosababisha magari yaliyokuwa yakielekea au kutoka Lamu, Garissa, Malindi na Mombasa kusimama. “Nimetoka Malindi nikielekea Lamu kupeleka abiria. Nilifika hapa saa moja asubuhi lakini hadi sasa bado tumekwama,” alisema dereva Joseph Kahindi. Bw Skanda, alisema hatua ya maafisa wa polisi wa kituo cha Gamba-Garsen kupuuza amri ya Mahakama Kuu ni dharau kwa Katiba, sheria na mamlaka ya mahakama. “Hakuna afisa aliye juu ya sheria. Amri za mahakama si mapendekezo bali ni maagizo yanayopaswa kutekelezwa mara moja,” alisema Bw Skanda. Hadi saa sita mchana, mamia ya wasafiri walikuwa bado wamekwama Minjila huku magari yakiendelea kufunga barabara. Maeneo yaliyoguswa na amri hiyo ni pamoja na sehemu za Lamu na Tana River kama Holugho, Galmagala, Sanagilu, Masalani, Ijara, Hola, Garsen, Kipini, Kiunga na mpaka wa Ishakani/Dar es Salaam.
Original story
Continue reading at Taifa Leo (Swahili)
taifaleo.nation.co.ke
Summary generated from the RSS feed of Taifa Leo (Swahili). All article rights belong to the original publisher. Click through to read the full piece on taifaleo.nation.co.ke.
