skipToContent
🌐All

UFUGAJI: Mtindo wa kisasa wa kutunza ndama anapozaliwa kuzuia vifo na maradhi

Taifa Leo (Swahili) Global
UFUGAJI: Mtindo wa kisasa wa kutunza ndama anapozaliwa kuzuia vifo na maradhi
HARAKATI za ufugaji, zinamhitaji mfugaji wa ng'ombe kutumia utaratibu na kanuni bora ili kutengeneza kizazi kizuri cha mifugo wake kwa siku zijazo. Harakati hizi zinajumuisha pia ukumbatiaji wa teknolojia za kisasa badala ya kutumia mbinu za kizamani ambazo zimepitwa na wakati. Aidha, utunzaji huangazia mambo mbalimbali kama vile hatua za ukuaji ambazo humsaidia mkulima kuhifadhi rekodi za malisho, afya, kiwango cha uzalishaji na soko la mazao yake. Akilimali ilipozuru eneo la Lanet Kaunti ya Nakuru, ilikutana na mkulima mwenye uzoefu wa muda mrefu, Francis Mwangi. Anasema ndama wanatakiwa kutengenezewa mazingira yao maalum. Anasema ili wakulima wadogo vijijini waweze kujikomboa kiuchumi, wakulima wanatakiwa kuendesha ufugaji kwa njia za kisasa. Kwa mfano wanapokama, wanaweza kutumia mashine au kufuga spishi za kisasa ambazo zinafahamika kwa kuzalisha lita nyingi za maziwa kila siku. Kulingana na Mwagi, ng'ombe walioboreshwa huwa wamegawika kwenye makundi mawili ambapo kuna wale wa nyama na wa maziwa. Akilimali inaangazia wale wa maziwa katika makala haya. Mwangi anawashauri wakulima kuwa mbali na kuendesha kilimo cha ufugaji wa ng'ombe kisasa, mkulima asiache teknolojia hizi zimwendeshee kilimo. “Anaweza kuwa na tarakilishi za kuhifadhi taarifa muhimu za mifugo wake, kamera za CCTV na simu ya mkononi,” asema. Kwa kutumia mfumo wa ‘calf pen’ ndama anaweza kutenganishwa na kundi la mifugo wengine. “Hatua hii inalenga kuhakikisha kuwa ndama anapatiwa mahitaji yote ya kimsingi kama vile dawa za kuzuia maambukizi ya viini vya magonjwa mara baada ya kuzaliwa.” Anasema mfumo huu wa kisasa pia humsaidia ndama aanze kujifunza namna ya kula majani laini ya vyakula ambavyo mara nyingi huwa ni mseto wa chakula cha wanga. Aidha, hapa ndama atapatiwa maziwa ya kwanza kutoka kwa mama mara baada ya kuzaliwa kwa lengo la kupata kinga ya mwili dhidi ya magonjwa. “Pia baada ya siku kadhaa anaweza kudhibitiwa bila kunyonya na hatimaye akaanza kujifunza kutafuna chakula pole pole badala ya kutegemea maziwa tu,” asema. Mwangi anasema kuwa mfumo huu umeboreshwa kwa sababu ufugaji wa ng'ombe wa maziwa. Kupitia mfumo huu, mbinu sahihi za kutunza ndama huzingatiwa kinyume na awali ambapo ndama alikuwa akitegemea maziwa ya mama kwa asilimia 100. Anasema ‘Calf Pen’ imejengwa kwa njia ya kipekee ambapo ndama huwa ametengenezewa, nafasi ya kutosha ili kumpatia uhuru wa kutembea na kujinyoosha bila kutangamana na ndama wengine. Isitoshe, sehemu hizo ­­­­­­­­­­­za kuweka ndama huwa zimegawanywa mara tatu na kuwekewa vifaa sawa na bakuli kwa ajili ya kubebea maji na chakula. Mpangilio huo husaidia ndama kupata lishe kwanza kabla ya kukamia maji, bila kusahau kuwa sehemu yao ya kukaa inafaa kusafishwa mara mbili kwa siku ili kuondoa samadi. Kwa upande mwingine, anasema kuwa sehemu hiyo ni sehemu muhimu katika utunzaji wa ndama kwa sababu husaidia kuhifadhi historia ya awali ya mifugo. Pia ni katika sehemu hii ambapo ndama huwekewa alama sikioni (ear tag), kipande ambacho huwekwa katika sikio la ndama ili kufuatilia mienendo yake.
Share
Original story
Continue reading at Taifa Leo (Swahili)
taifaleo.nation.co.ke
Read full article

Summary generated from the RSS feed of Taifa Leo (Swahili). All article rights belong to the original publisher. Click through to read the full piece on taifaleo.nation.co.ke.