“KWA miaka mingi, ufumaji wa vikapu umekuwa uti wa mgongo wa maisha ya wanawake wengi katika jamii mbalimbali nchini Kenya na sehemu nyingine za Afrika. Mbali na kuwa chanzo cha mapato, sanaa hiyo ya jadi imekuwa njia ya kuhifadhi mila, tamaduni na historia ya jamii kutoka kizazi kimoja hadi kingine. Kutoka kwa nyanya hadi kwa mabinti zao, na sasa kwa kizazi cha vijana wa leo, ufumaji umeendelea kupewa nafasi muhimu katika jamii. Huko Turkana, utamaduni huo bado unadumu licha ya mabadiliko ya teknolojia na maisha ya kisasa. Miongoni mwa wanawake wanaoendeleza sanaa hiyo ni Ruth Acharait, mama kutoka Lodwar ambaye ameifanya kazi ya ufumaji kuwa nguzo ya kujikimu na kuhifadhi utamaduni wa jamii yake. Acharait ni mwanachama wa makundi mawili ya kijamii – Lodwar Baskets na Beads Youth Group – yaliyoanzishwa mwaka 2013 kwa lengo la kusaidia wanawake na vijana kiuchumi kupitia ufumaji wa vikapu na bidhaa za shanga. Mfumo wa kidijitali Akiwa na zaidi ya miaka 50, anasema ufumaji ni urithi waliopokea kutoka kwa mababu zao. “Ni kazi tuliyoachiwa na mama zetu na wao pia walifunzwa na mama zao. Hivyo tunaendelea kuitunza ili isiishe,” anasema. Kwa miaka mingi, vikapu hivyo vilifumwa kwa kutumia majani ya doum palm na papyrus reed grass , kisha kurembeshwa kwa shanga za rangi mbalimbali. Wakati huo, masoko yalitegemea sana mfumo wa kauli ya mdomo au soko la kawaida vijijini. Lakini ujio wa teknolojia ya kidijitali umebadili sura ya biashara hiyo. Leo hii, wanawake hao wanatumia majukwaa ya kijamii kama WhatsApp, Facebook, Instagram, TikTok na X kufikia wateja ndani na nje ya Kenya. “Tunatumia intaneti kuonyesha kazi zetu na kuwafikia wanunuzi wengi zaidi. Wateja sasa wanatuona hata kutoka mataifa ya nje,” Acharait anasema. [caption id="attachment_188257" align="aligncenter" width="300"] Baadhi ya vikapu maridadi vilivyofumwa na Ruth Acharait. Picha|Sammy Waweru [/caption] Kulingana naye, matumizi ya mitandao ya kijamii yamechangia ukuaji mkubwa wa makundi hayo. Beads Youth Group ilianza na wanachama 10 pekee mwaka 2013, lakini sasa ina zaidi ya wanachama 20. Nalo kundi la Lodwar Baskets limepanuka kutoka wanachama watano waanzilishi hadi kufikia wanachama 47. Mauzo kuongezeka Ukuaji huo umeenda sambamba na ongezeko la mauzo. Ingawa hakutaja kiwango halisi cha mapato yao, Acharait anasema mauzo ya vikapu yameongezeka maradufu tangu waanze kutumia mfumo wa kidijitali. “Awali tulikuwa tunauza kiwango kidogo sana cha vikapu kwa mwezi, lakini sasa mauzo yameongezeka sana kwa sababu tunafikia watu wengi kupitia mitandao,” anaeleza. Mbali na kuuza bidhaa, wanawake hao pia wamejifunza kutumia simu tamba (smart phones) kupiga picha na video za kazi zao, kuzihariri na kuzisambaza mitandaoni ili kuvutia wateja. “Ndio, sisi ni watu wa kizazi cha zamani, lakini watoto wetu wametufunza kutumia teknolojia. Sasa tunaweza kupakia picha na video za vikapu vyetu mtandaoni na kupata wateja,” anasema huku akitabasamu. Kadri biashara inavyokua, ndivyo ubunifu unavyoongezeka. Hapo awali walitumia rangi moja au mbili za shanga kupamba vikapu, lakini sasa wanatumia mchanganyiko wa rangi mbalimbali zinazovutia soko la kisasa. Baadhi ya vikapu pia hufumwa kwa rangi za bendera ya Kenya, jambo ambalo limevifanya kuvutia wanunuzi wa kimataifa. [caption id="attachment_188258" align="aligncenter" width="300"] Ruth Acharait, mama kutoka Lodwar akifungua kapu. Picha|Sammy Waweru [/caption] Ufadhili kuboresha sanaa Kwa Acharait, teknolojia si tishio kwa tamaduni, bali ni daraja linalosaidia utamaduni kufikia ulimwengu. “Huko ndiko dunia inaelekea. Kila mtu yuko mtandaoni sasa, kwa hivyo nasi lazima twende na wakati,” anasema. Makundi hayo ni miongoni mwa yaliyonufaika kupitia mradi wa IMARA uliotekelezwa na World Vision Kenya kwa ushirikiano na Ubalozi wa Sweden. Mradi huo ulilenga zaidi ya watu 73,000 katika kaunti tisa za maeneo kame na nusu-kame (ASAL), ikiwemo Turkana. Mbali na kusaidia juhudi za kufufua ardhi iliyoharibika na kuhifadhi mazingira, mradi huo pia ulisaidia vikundi vya kijamii vinavyoendeleza biashara ndogondogo na kuhifadhi tamaduni za jamii zao. Programu hiyo ya miaka saba, iliyofadhiliwa na Serikali ya Sweden kupitia Swedish International Development Cooperation Agency (Sida) kwa gharama ya SEK211 milioni, sawa na takriban Sh3.22 bilioni, ilikamilika Aprili 2026. Kwa wanawake wa Turkana kama Ruth Acharait, mabadiliko ya kidijitali hayajaongeza kipato pekee, bali pia yamehakikisha kuwa sanaa ya jadi ya ufumaji vikapu inaendelea kuishi katika kizazi cha sasa na kijacho.
Original story
Continue reading at Taifa Leo (Swahili)
taifaleo.nation.co.ke
Summary generated from the RSS feed of Taifa Leo (Swahili). All article rights belong to the original publisher. Click through to read the full piece on taifaleo.nation.co.ke.
