skipToContent
🌐All

Ulinzi na NIS zamegewa Sh310 bilioni, matumizi makubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa

Ulinzi na NIS zamegewa Sh310 bilioni, matumizi makubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa
WIZARA ya Ulinzi na Huduma ya Kitaifa kuhusu Ujasusi (NIS) zitapokea jumla ya Sh310 bilioni kwenye bajeti ya 2026, kiasi ambacho ni cha pili kikubwa zaidi baada ya Tume ya Huduma kwa Walimu (TSC), iliyo na Sh422.7 bilioni, kulingana na stakabadhi za bajeti zilizowasilishwa bungeni. Kiasi hicho kimepita kwa mbali mgao wa miaka iliyotangulia huku ripoti za ukaguzi wa hesabu za umma zikimulika matumizi ambapo Afisi ya Mdhibiti wa Bajeti (CoB) ilizua maswali kuhusu viwango vya matumizi ya hela katika baadhi ya miradi muhimu. Wizara ya Ulinzi na NIS zinajumuisha sekta ya ulinzi kitaifa zenye wajibu wa kuhakikisha usalama wa nchi dhidi ya tishio kutoka ndani au nje ya mipaka ya Kenya, kulinda nchi na kusaidia walinda usalama kudumisha amani na utulivu. Kwa mujibu wa makadirio ya 2026/2027 yaliyowasilishwa katika Bunge la Kitaifa, Wizara ya Ulinzi imetengewa Sh250.02 bilioni, kiasi ambacho ni karibu maradufu cha iliyotengewa miaka mitatu iliyopita, huku NIS ikipata Sh58.62 bilioni. Lakini hata kabla ya mwaka wa kifedha wa 2026/27 kuanza kwa Wizara, Idara na Taasisi (MDAs) ili kuanza kutumia fedha ilizogawiwa na Bunge la Kitaifa, NIS tayari inamezea mate bajeti ya ziada, hivyo kukiuka nidhamu kuhusu matumizi ya fedha kuambatana na Sheria kuhusu Usimamizi wa Fedha za Umma (PFM). “Ili kuangazia kikamilifu changamoto hizi, NIS itashirikiana na Hazina Kuu ili kupata fedha za ziada,” ikasema stakabadhi hiyo. Licha ya kuongezewa raslimali, Wizara ya Ulinzi inazidi kukabiliwa na changamoto anuai ikiwemo maendeleo ya kasi kuhusu teknolojia za jeshi ambayo yamesababisha kiwango cha juu cha vifaa kupitwa na wakati na gharama ya juu ya ukarabati, mipaka hatari, upungufu wa wafanyakazi miongoni mwa mengine. Bajeti ya 2026/27 iliyoandaliwa na Hazina Kuu inaashiria Wizara ya Ulinzi ilitengewa Sh139 bilioni katika mwaka wa kifedha 2022/23, Sh159.1 bilioni katika mwaka wa kifedha wa 2023/24 na Sh179.7 bilioni katika bajeti ya 2024/25. Ripoti ya Mkaguzi Mkuu Nancy Gathungu inaashiria kuwa katika bajeti ya 2024/25, Wizara ya Ulinzi haikuchukua hatua ya kutekeleza mapendekezo kuhusu matumizi ili “kuimarisha imani na kuhakikisha kuwa fedha zinatumiwa kwa uwajibikaji pasipo kuhujumu usalama wa nchi.”
Share
Original story
Continue reading at Taifa Leo (Swahili)
taifaleo.nation.co.ke
Read full article

Summary generated from the RSS feed of Taifa Leo (Swahili). All article rights belong to the original publisher. Click through to read the full piece on taifaleo.nation.co.ke.