skipToContent
🌐Secondary

UPELELEZI: Moto ulioua 16 uliwashwa makusudi

Taifa Leo (Swahili) Global
UPELELEZI: Moto ulioua 16 uliwashwa makusudi
MOTO uliosababisha vifo vya wanafunzi 16 katika shule ya Utumishi Girls Senior School, Gilgil na wengine 79 kujeruhiwa, ulipangwa na kutekelezwa kimakusudi, uchunguzi wa awali wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) umebaini. Hapo jana, ilibainika kuwa huenda mkasa huo ulioshtua taifa ulipangwa na baadhi ya wanafunzi waliokuwa wakilalamikia kile walichodai kuwa ukali wa wasimamizi wa shule. Ufichuzi huo ulijiri huku maafisa wa DCI wakiwakamata wanafunzi wanane wanaodaiwa kuwa vinara wa shambulizi hilo la kuchoma bweni moto. Katika taarifa yake, DCI ilisema baada ya uchunguzi wa kina, wanafunzi hao wanane wamehusishwa moja kwa moja na kupanga na kutekeleza tukio hilo lililosababisha vifo na majeraha kwa wanafunzi wengi. “Tumefanya mahojiano ya kina na wanafunzi, walimu pamoja na mashahidi wengine na pia kupitia picha za kamera za CCTV. Uchunguzi wa awali umebaini wanafunzi wanane kama wanaoweza kuwa walipanga na kutekeleza tukio hilo la uchomaji moto,” ilisema sehemu ya taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa DCI Mohamed Amin. “Wasichana hao wanane wamekamatwa na kwa sasa wanazuiliwa na polisi. Maafisa wa upelelezi wanaendelea kurekodi taarifa na kuchambua ushahidi wote uliopo ili kubaini matukio na sababu ya mkasa huo,” iliongeza taarifa hiyo. Wapelelezi walianza uchunguzi Alhamisi baada ya manusura wa mkasa huo kudai kuwa moto huo ulianzishwa na wanafunzi wenzao waliowasha moto kwenye godoro. Walieleza kuwa moto huo ulisambaa kwa kasi na kuliteketeza bweni lote la Meline Waithera na kusababisha vifo pamoja na majeraha. Uchunguzi kuhusu chanzo cha moto huo ulikabidhiwa kitengo cha mauaji cha DCI. Maafisa hao wa uchunguzi wanajumuisha wataalamu wa eneo la uhalifu, maafisa wa utafiti wa uhalifu na ujasusi, wataalamu wa picha za upelelezi, sauti pamoja na wataalamu wa DNA. Wapelelezi wanataka kubaini chanzo cha moto huo, kuchunguza namna ulivyosambaa, kubaini kilichotumika kuwasha moto huo na pia kuchunguza mfumo wa umeme wa shule ili kufahamu chanzo halisi cha mkasa huo. Wanafunzi hao wanatarajiwa kufikishwa mahakamani wiki ijayo. Huku taifa likiendelea kuomboleza, uchunguzi wa awali umeonyesha kuwa mpango ulianza kusukwa zaidi ya wiki moja kabla ya mkasa huo. Imebainika kuwa wanafunzi hao waliingiza mafuta ya taa shuleni na kuyatumia kuwasha moto ulioua wenzao na kuwaacha wengi wamejeruhiwa. Taifa Leo imebaini kuwa wanafunzi hao walitumia fursa ya kutokuwepo kwa msimamizi wa mabweni wa shule kuingiza mafuta hayo ya taa ndani ya shule na kisha kuwasha godoro moto. Imebainika pia kuwa huenda wanafunzi hao walifunga mlango wa bweni baada ya kuwasha moto huo. Taifa Dijitali imefahamu kuwa kulikuwa na uvumi kuhusu mgomo uliokuwa ukipangwa shuleni humo wiki moja kabla ya mkasa lakini usimamizi wa shule haukuchukua hatua zozote kuzuia hali hiyo. Baadhi ya walimu walikuwa wamepata taarifa kuhusu mgomo uliokuwa ukipangwa lakini hawakuchukua hatua. “Tulianza kusikia uvumi kuhusu mgomo wiki moja kabla. Baadhi ya wanafunzi wa kidato cha tatu walikuwa wakisema watachoma shule ikiwa malalamishi yao hayatasikilizwa. Walikuwa wakilalamikia chakula kibaya na ukali wa usimamizi wa shule,” alisema mwanafunzi mmoja manusura. Aliongeza kuwa usiku kabla ya moto, walilala saa tatu usiku na taa zilizimwa kama kawaida katika mabweni ya Stanford na Oxford. “Tuliamshwa na mmoja wetu aliyepiga kelele kuwa bweni linaungua. Kulikuwa na taharuki kubwa huku kila mmoja akijaribu kujiokoa,” alisema. Mwanafunzi huyo alisema moto ulikuwa tayari umeenea sana kufikia wakati walipopata tahadhari. “Njia ya kutokea ilikuwa tayari imezingirwa na moto huku moshi ukiwa mwingi. Wengine walilazimika kuruka kupitia madirishani kujiokoa. Mimi niliruka dirishani na kuvunjika mguu,” alisema. Mzazi mmoja ambaye binti yake alinusurika alisema moto huo ulianzia katikati ya bweni lililokuwa na wanafunzi wa Grade 10, kidato cha tatu na kidato cha nne. “Mwanangu aliniambia kuwa moto ulianza kwenye kitanda kilichokuwa katikati ya bweni kabla ya kusambaa kwa kasi. Kwa kuwa kitanda chake kilikuwa karibu na mlango, aliweza kutoroka salama,” alisema mzazi huyo. Mwanafunzi mwingine alisema alilazimika kuruka dirishani kuokoa maisha yake. “Moto ulianza karibu na sehemu yangu ya kulala. Nilipoona siwezi kutoka kupitia mlango, niliruka dirishani na kujeruhiwa miguu na mikono,” alisema mwanafunzi huyo aliyepatiwa matibabu katika hospitali ya St Mary’s. Mkasa huo umefichua ukiukaji mkubwa wa kanuni za usalama za Wizara ya Elimu huku ikibainika kuwa bweni hilo lilikuwa limejaa wanafunzi kupita kiasi. Taifa Dijitali imebaini kuwa bweni hilo halikuwa na milango ya dharura huku madirisha yake yakiwa na vyuma. Bweni hilo lilikuwa na milango miwili pekee ya kutokea huku mmoja ukiwa umefungwa kabisa, hali iliyozuia wanafunzi kutoroka kwa haraka. Mlango uliobaki pia ulikuwa umefungwa wakati wa mkasa huo. Imebainika pia kuwa moto huo ulisambaa haraka kutokana na matumizi ya mbao zilizotumika kugawa sehemu za bweni. Wakati mkasa huo ulipotokea, mlango wa bweni ulikuwa umefungwa kutoka ndani na funguo hazikuweza kupatikana kwa haraka jambo lililochelewesha juhudi za uokoaji. Kutokana na mkasa huo, Wizara ya Elimu imevunja Bodi ya Usimamizi ya shule hiyo baada ya kubainika kuwa shule ilikiuka kanuni za usalama. Waziri wa Elimu Julius Ogamba alisema moto huo ulizuka saa sita usiku na kusababisha vifo pamoja na uharibifu wa mali. Alisema shule hiyo ilikuwa na wanafunzi 815 huku 809 wakiwa shuleni wakati wa mkasa huo. Ripoti ya polisi ilionyesha kuwa ilichukua zaidi ya saa mbili kwa vikosi vya zimamoto kutoka Naivasha, maafisa wa KDF, ASTU, NYS pamoja na Shirika la Msalaba Mwekundu kuzima moto huo.
Share
Original story
Continue reading at Taifa Leo (Swahili)
taifaleo.nation.co.ke
Read full article

Summary generated from the RSS feed of Taifa Leo (Swahili). All article rights belong to the original publisher. Click through to read the full piece on taifaleo.nation.co.ke.