“Uhuru wa Kenyataa, liweza tenda makuu, Taifa weza kung'aa, nchi piga hatua kuu, Mambo yenye umang'aa, 'liisha kwa njia kuu, Uhuru ni kiongozi, alitenda mema nchini. Watahiniwa kuweza, lipiwa za mitihani. Hilo jambo 'liongeza, walofanya mutihani, Alisaida punguza, mzigo kwa wazazini, Uhuru ni kiongozi, alitenda mema nchini. Gharama karo shuleni, iliweza kupungua, Uhuru alifanyeni, milango heri fungua, Elimu ya Kenya nchini, 'liweza vizuri kua, Uhuru ni kiongozi, alitenda mema nchini. Katika miundombinu, barabara weza jengwa, Barabara kawa tunu, kwa njia zilimopangwa, Barabara wekwa winu, katoa sura ya jangwa, Uhuru ni kiongozi, alitenda mema nchini. Kajenga reli kisasa, toka pwani hadi bara, Nchi ikawa na usasa, pamoja na nzuri sura, Ujenzi wenye kisasa, ulifanya Kenya bora, Uhuru ni kiongozi, alitenda mema nchini. Usambazaji wa stima, uliweza wekwa nchini, Akina baba na mama, wakapanda toka chini, Umeme ni nguzo kama, weza inua wa chini, Uhuru ni kiongozi, alitenda mema nchini. Kwa wizara ya afya, bima ilikuwa nzuri, Linda mama ya afya, 'kajifungua vizuri, Wanafunzi na afya, 'liwalinda njia nzuri, Uhuru ni kiongozi, alitenda mema nchini. Vituo vyenye huduma, vilirahisisha mambo, Wananchi pata huduma, nchi ikawa nzuri umbo, Vitambulisho huduma, shika kwa rahisi jambo, Uhuru ni kiongozi, alitenda mema nchini. Aliazima umoja, miongoni mwa wakenya, Alitaka Kenya moja, kwa kunganisha wakenya, Wananchi wawe wamoja, kwenye taifa la Kenya, Uhuru ni kiongozi, alitenda mema nchini. Na aliweza ungana, wa siasa mahasimu, Ili anza kupambana, uongozi wa kuzimu, Aliweza kupangana, na vongozi nchini humu, Uhuru ni kiongozi, alitenda mema nchini. JOSHUA OMACHE, CHUO KIKUU CHA KIBABII Bubu Kunena Mbona mnakunja sura, mlijua mwisho wake? Naona imewakera, bubu kupata la kwake, Si siri mwagaragara, na mito kupiga teke, Kwani bubu akinena, ni baraka au bina? Katu haiwezekani, wengine wamechangia, Bubu tu anene nini, mjadala 'kaingia, Kwani hawana imani, hata ya kujitungia? Kwani bubu akinena, ni baraka au bina? Wengine washangilia, Wakosatonge na bubu, Mwanga 'mewamulikia, katika giza na tabu, Ni baraka kwao pia, bubu kuwapa majibu, Kwani bubu akinena, ni baraka au bina? Mfisadi na pwaguzi, ni bina wameambiwa, 'Mevunjika zao ngazi, siri zinafichuliwa, Ujanja wao wa juzi, bubu sasa atongowa, Kwani bubu akinena, ni baraka au bina? Bubu sasa u motoni, kashikwa na wenye siri, Roho yake mkononi, hukumu akisubiri, Kumbe kunena ni shani, kunena kumbe shubiri, Kwani bubu akinena, ni baraka au bina? Mwacheni aseme lake, mwacheni amwaye yote, Lilo'funga moyo wake, mara moja alikate, Wano'cheka na wacheke, wano'teta na watete, Kwani bubu akinena, ni baraka au bina? AUSTINE O ONYANGO ‘MALENGA WA MTO NILE’ CHUO KIKUU CHA JARAMOGI (JOOUST) Bei ya mafuta Mafuta yamepanda, kama mwewe angani, Bei imekuwa kubwa, haina hata thamani, Mifuko ina mashimo, imetoboka jamani, Gari sasa ni sanamu, limebaki uwanjani. Nakwenda kituoni sasa, na hofu tele moyoni, Gharama zinanitesa, nina huzuni jamani, Kila siku ni mkasa, mfuko hauna nguvu, Gari sasa ni sanamu, limebaki uwanjani. Mshahara hautoshi, lita mbili ni gharama, Maisha hayashikiki, tunabaki kusononeka, Hata safari hazikwendi, tunabaki tumerama, Gari sasa ni sanamu, limebaki uwanjani. Barabara ziko wazi, magari yamepungua, Kupaki ndiyo uamuzi, jua likituchoma, Hali hii ni dhiki kuu, kamba inatubana, Gari sasa ni sanamu, limebaki uwanjani. Enyi wenye mamlaka, tazameni hali yetu, Mioyo imechoka sana, kipato ni duni kwetu, Bei ishuke haraka, ipone mitambo yetu, Gari sasa ni sanamu, limebaki uwanjani. Hatima nafunga tamati, kwa kilio na huzuni, Maisha yanatuyumba, tunaishi kwa huzuni, Tunaomba bei ishuke, turudi barabarani, Gari sasa ni sanamu, limebaki uwanjani. DENNIS KIOKO ‘MHARIRI CHIPUKIZI’ CHUO KIKUU CHA KITEKNOLOJIA CHA MURANG’A Wavyele nambie Machozi yatirirka, huzuni na sikitiko Moyoni nasikitika, huzuni mnijazako Watoto wadogo kuoleka, wapata jiko Wavyele wangu mnambie, haya maisha gani? Sikilizeni makini, ushauri mpewapo Shule zipo likizoni, wanenu wapoteapo Wazazi mwanyamazani, wenu waharibikapo? Wavyele wangu mnambie, haya maisha gani? Swali niliulizalo, jibu lake silipati Kote jini nilizungukalo, jibu silipati Somo liirudiwalo, wanafunzi hawapati Wavyele wangu mnambie, haya maisha gani? Shule zifunguliapo, wako wapi wanafunzi? Darasani wafikapo, hakunako wanafunzi Wamekuwa wakifiapo, kidondani kama nzi Wavyele wangu mnambie, haya maisha gani? Nasaha mwaziweka mbali, watoto hamwapi Hawatulii kwenye Manzili, wangali kutapi Wamekuwa tapeli, moyo wenu haumpapi Wavyele wangu mnambie, haya maisha gani? Fumbueni macho yenu, mwangalie siku kesho Wakilalamika wenu, hawaangalii kesho Mwajiaribia yenu, hakuna wetu wa kesho Wavyele wangu mnambie, haya maisha gani? Tamati nafikia, wazazi na watoto wenu Ningali nalalamikia, usalama wa wenu Mashauri mwafukia, hawahitaji wanenu? Wavyele wangu mnambie, haya maisha gani? ROMANO NDUYO Nimekombolewa Nimekuwa kanisani, kumuomba Mungu wangu Na sadaka mfukoni, kushukuru Mungu wangu Nikatia kikapuni, fungu la kipato changu Leo nimefunguliwa, Mimi si mfungwa tena! Mimi si mfungwa tena, zimefutwa dhambi zangu Nimetubu kwa kunena, kumweleza Mungu wangu Nikaomba kufanana, na Yesu Mwokozi wangu Leo nimefunguliwa, sitotenda dhambi tena Sitotenda dhambi tena, siendelei kutusi Nitakoma kupigana, iniondoke mikosi Nimezivunja laana, tena sina wasiwasi Leo nimefunguliwa, nikawa kiumbe mpya Nikawa kiumbe kipya, sitaki tena kulewa Nikapewa mwili mpya, dhambini kukombolewa Nikajazwa nguvu mpya, na pia kubarikiwa Leo nimefunguliwa, Mimi nimebadilika! Nifikapo ukingoni, natua yalo moyoni Nawaombea wendani, pia mtoke dhambini Mmwondokee shetani, Mungu awasameheni Mimi nilitubu kwake, akanipa msamaha JAPHETH NZOMO ‘ZAO LA HEKIMA’ CHAKIMUT Saa ya bosi Siku yangu imeisha, ni salama salimini Usiku wote 'mekesha, hapa kwetu kituoni Sare nimezirudisha, niende zangu nyumbani Ni masaa ya bosi, brigedia anafika Ni masaa ya bosi, brigedia anafika Leo hataki matusi, wallahi mebadilika Menilipia teksi, mwenzenu ninashtuka Bosi amekuwa mwema, wallahi siamini Bosi amekuwa mwema, wallahi siamini Leo anipa heshima, mimi nashindwa kwa nini Kapenda yangu huduma, au kenda msikitini Wacha nifike nyumbani, kesho tajua ukweli Wacha nifike nyumbani, kesho tajua ukweli Nimejilaza kochini, nabishana na akili Mesegi ipo simuni, menitumia nauli Nifike zamu kazini, ataka kwenda shughuli Nifike zamu kazini, ataka kwenda shughuli Amenipa usukani, na kibandani silali Ninajihisi ndotoni, machweo anawasili Naenda zangu nyumbani, anaingia zamuni Naenda zangu nyumbani, anaingia zamuni Leo silali kochini, naenda zangu bedini Macho yangu siamini, pengine nipo ndotoni Hii saa yake bosi, kwangu yafanya nini? Hii saa yake bosi, kwangu yafanya nini? Ni saa ya almasi, limewekwa beserani Mjinga ninajihisi, mambo haya mambo gani? Mke wangu namuita, upesi aja chumbani Mke wangu namuita, upesi aja chumbani Moyo wangu wanitweta, saa ipo mkononi Kuona kajikunyata, kazirai sakafuni Niko na yeye wodini, apone anipe jibu EZEKIEL NZEKE ‘USTADH KARMA’ MURANG’A Niombeeni Kwa nudhuma naandika, chozi likitiririka, Nguvu zinanikatika, na mwili kutetemeka, Ukweli usokanika, maini unaokata, Sitaki mulielie, niombeeni mwenzenu. Mtima wanishituka, kila ninapokumbuka, Kwamba siku itafika, duniani kupatoka, Nirudi kwake Rabuka, ulimwengu kuutoka, Wala msilielie, niombeeni mwenzenu, Siku itakapofika, roho yangu ikang'oka, Muache kuweweseka, machozi yakawatoka, Nifunikeni haraka, mwilini kusitirika, Kamwe msilielie, niombeeni mwenzenu. Ndugu nanyi kina kaka, mikono mujenishika, msije nje kutoka, mabaya yakanifika, Muilinde yangu shuka, hadi masaa kufika, Wala msilielie, muniombee mwenzenu. Sitawa na mamlaka, ya kuswali kwa hakika, Basi mutakaofika, muniombee baraka, Nende ikuta fanaka, ya dua zenu kifika, Yani msilielie , muniombee mwenzenu. Kisha msiche kutoka, nyumbani kwenu kufika, Riziki mwendeisaka, na mengine kadhalika, Uwaondoke wahaka, kiwewe kuwaepuka, Tena msilielie, muniombee mwenzenu. Na wakwangu wahibaka, wazazi na kina kaka, Kina dada mewatoka, aushi mekamilika, Munitolee na zaka, naimani itafika, Jama msilielie, muniombee mwenzenu. SALIM MWASUNA ‘MWASUNA MSHAIRI’ KWALE Mwambieni Shangazi! Mwambieni shangazi, salamu nimemtumia, Kila kucha na machweo, moyo alinichukia, Alitamani tuanguke, huzuni itutawale, Kwa mkono wa Mungu, mafanikio yametimia, Mungu amenisaidia, mafanikio yamefika. Kwa hila na fitina, njama alizozipanga, Akataka tushindwe, maisha yawe matanga, Lakini nuru ya Mola, gizani ikaangaza, Kwa neema ya Mwenyezi, tumefanikiwa sana, Mungu amenisaidia, mafanikio yamefika. Alitaka tuwe duni, tuishi kwa shida na dhiki, Tuonekane wa chini, tukose hata marafiki, Lakini Mungu wa haki, ametupa ushindi, Leo tunasimama imara, kwa rehema zake tele, Mungu amenisaidia, mafanikio yamefika. Mwambieni shangazi, wivu si njia ya heri, Moyo wa husuda, haujengi kesho njema, Mungu ndiye mgawaji, riziki na kila kheri, Nami ameninyanyua, akanitoa pabaya sana, Mungu amenisaidia, mafanikio yamefika. Leo nyumba imesimama, na watoto wasoma, Baraka zimeongezeka, kwa rehema zisizokoma, Si kwa nguvu zangu, wala akili za binadamu, Ni Mungu aliyefanya, jina lake litukuzwe daima, Mungu amenisaidia, mafanikio yamefika. Sitetemeshwi na maneno, wala vitisho vya watu, Nina ulinzi wa Mola, siogopi wala katu, Mwambieni kwa heshima, safari si bahati Ni Mungu amenifikisha, kwenye ushindi wa haki, Mungu amenisaidia, mafanikio yamefika. DENNIS KIOKO ‘MHARIRI CHIPUKIZI’ CHUO KIKUU CHA KITEKNOLOJIA CHA MURANG’A
Original story
Continue reading at Taifa Leo (Swahili)
taifaleo.nation.co.ke
Summary generated from the RSS feed of Taifa Leo (Swahili). All article rights belong to the original publisher. Click through to read the full piece on taifaleo.nation.co.ke.
