skipToContent
🌐All

Ushindi kwa Arsenal PGMOL ikitetea uamuzi wa kukataa bao la West Ham

Taifa Leo (Swahili) Global
Ushindi kwa Arsenal PGMOL ikitetea uamuzi wa kukataa bao la West Ham
CHAMA cha waamuzi wa soka Uingereza (PGMOL) jana kilitetea uamuzi wa kufuta bao la kusawazisha la dakika za mwisho la West Ham United dhidi ya Arsenal kwenye mechi ya Ligi Kuu Uingereza (EPL). Mechi hiyo ya Jumapili ilikuwa na umuhimu mkubwa kwa timu zote mbili, huku West Ham wakipambana kujinusuru kushuka daraja na Arsenal wakisaka ubingwa wa ligi. West Ham walidhani wamejinyakulia pointi muhimu baada ya Callum Wilson kufunga kufuatia kona katika dakika za majeruhi. Hata hivyo, baada ya utathmini wa VAR, mwamuzi Chris Kavanagh aliitwa kuangalia tukio hilo kwenye runinga kabla ya kufuta bao hilo. Hatua hiyo ilitokana na kosa lililofanywa na Pablo dhidi ya kipa wa Arsenal David Raya kabla ya Wilson kufunga. Hatua hiyo ilihakikisha Arsenal wanashinda mechi hiyo 1-0 na kujikusanyia pointi zote tatu muhimu. Wachanganuzi wa soka wameutaja uamuzi huo kuwa mkubwa zaidi wa VAR katika EPL tangu mfumo huo uanze kutumika mwaka 2019. “Je, lilikuwa kosa dhidi ya kipa? Bila shaka ndiyo,” alisema mkuu wa PGMOL Howard Webb kwenye kipindi cha televisheni cha Match Officials Mic’d Up. “Tumekuwa tukisema msimu mzima, ikiwemo katika mikutano ya kabla ya msimu na wachezaji, kwamba ikiwa kipa atazuiwa na mchezaji wa timu pinzani kwa kushikwa au kuvutwa mikono kiasi kwamba hawezi kufanya kazi yake, basi hilo litachukuliwa kuwa kosa.” akaongeza. “Raya hakuweza kufanya kile ambacho angefanya kawaida katika hali hiyo, kushika mpira au kuupiga ngumi kuondoa hatari, hivyo VAR waliingilia na kufikia uamuzi sahihi,” aliongeza. Makosa mengine yaliyoweza kutokea yalichunguzwa pia na timu ya VAR, lakini Webb alikubaliana na uamuzi kwamba kosa muhimu zaidi lilikuwa lile dhidi ya kipa. Kinaya ni kwamba Arsenal wenyewe wamekuwa wakikosolewa msimu huu kwa kuwavuruga makipa wakati wa mipira ya kona. Ushindi wa Arsenal uliiweka kileleni mwa jedwali kwa tofauti ya pointi tano dhidi ya Manchester City, ambao walikuwa wacheza mechi yao ya kiporo dhidi ya Crystal Palace Jumatano usiku. Kwa upande mwingine, West Ham wanaendelea kubaki katika nafasi ya tatu kutoka mwisho, wakiwa pointi mbili nyuma ya Tottenham Hotspur huku zikiwa zimesalia mechi mbili kabla ya msimu kumalizika.
Share
Original story
Continue reading at Taifa Leo (Swahili)
taifaleo.nation.co.ke
Read full article

Summary generated from the RSS feed of Taifa Leo (Swahili). All article rights belong to the original publisher. Click through to read the full piece on taifaleo.nation.co.ke.