skipToContent
🌐All

Viongozi wa Garissa waomba msamaha kwa mauaji Kitui

Viongozi wa Garissa waomba msamaha kwa mauaji Kitui
VIONGOZI kutoka Kaunti ya Garissa wameomba msamaha kufuatia mauaji ya kikatili ya mvulana wa miaka 14 na watu wengine 7, yaliyotokea Ukasi katika Kaunti ya Kitui na kuzua majonzi na maandamano katika mpaka wa kaunti hizo mbili. Akizungumza katika mkutano wa amani uliowaleta pamoja viongozi kutoka pande zote, Gavana wa Garissa, Nathif Jama, alisema tukio hilo ni la kusikitisha na lisilokubalika, akisisitiza kuwa jamii yake haipaswi kuhusishwa na vitendo vya watu wachache wanaokiuka sheria. “Kwa niaba ya watu wa Garissa, tunaomba msamaha kwa tukio hili la kusikitisha. Tunalaani vikali mauaji haya na tunasimama pamoja na familia ya marehemu katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo,” alisema. Viongozi wengine wa Garissa waliunga mkono kauli hiyo, wakieleza kuwa waliohusika na mashambulizi hayo ni watu wachache wasiowakilisha jamii nzima. Walisema ni muhimu kuepuka lawama za jumla ambazo zinaweza kuchochea chuki na kuendeleza mzunguko wa kisasi kati ya jamii zinazoishi katika mpaka wa kaunti za, Garissa, Tana River na Kitui. Wito wa amani ulitolewa sambamba na tahadhari kali dhidi ya mashambulizi ya kulipiza kisasi, ambayo yamekuwa yakichochea uhasama kati ya wakulima na wafugaji katika eneo hilo. Migogoro hiyo mara nyingi hutokana na ushindani wa rasilimali muhimu kama maji na malisho ya mifugo, hasa wakati wa ukame. Gavana wa Kitui, Julius Malombe, aliwataka viongozi na wananchi kuepuka kutoa kauli za uchochezi kufuatia mauaji katika maeneo ya mpakani kati ya Kitui na Tana River. Alisisitiza kuwa jamii za pande zote zimeishi kwa amani kwa miaka mingi na hazipaswi kuruhusu matukio ya watu wachache kuvuruga uhusiano huo na ujirani mwema. Dkt Malombe alisema Kitui na jamii za Kaskazini mwa Kenya zimekuwa zikisaidiana na kushirikiana kihistoria, hivyo ni muhimu kulinda umoja huo. Wakati huohuo, kamishn wa kaunti ya Kitui Erastus Mbui alisema jumla ya watu 15 kutoka Kaunti za Kitui na Tana River wameuawa tangu Machi 29 katika mfululizo wa mapigano kati ya wakulima na wafugaji wa ngamia. Waliouawa ni pamoja na mvulana aliyekatwa Ukasi Jumanne na wengine saba waliouawa katika eneo la Kwa Kamari, Kitui, Jumamosi iliyopita. Viongozi hao walisisitiza pia umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya jamii hizo mbili ambazo zimeishi pamoja kwa muda mrefu licha ya changamoto za mara kwa mara. Walisema historia ya ujirani mwema haipaswi kuharibiwa na matukio ya watu wachache wenye nia mbaya. Aidha, waliwahimiza maafisa wa usalama kuongeza kasi ya uchunguzi na kuhakikisha wahusika wa mauaji wanakamatwa na kufikishwa mahakamani. Waliahidi kushirikiana kikamilifu na serikali ya kitaifa na ya kaunti kurejesha hali ya amani na utulivu katika eneo hilo la mpakani. Wakati huohuo, viongozi walipendekeza kuanzishwa kwa mikakati ya muda mrefu ya kudhibiti migogoro ya wafugaji na wakulima, ikiwemo usimamizi bora wa malisho, vituo vya polisi mpakani na elimu ya amani kwa jamii za eneo hilo. Mkutano huo ulimalizika kwa wito wa pamoja wa kudumisha mshikamano, huku viongozi wakisisitiza kuwa haki kwa Joseph Mutemi lazima ipatikane bila kuchochea mivutano zaidi kati ya jamii jirani.
Share
Original story
Continue reading at Taifa Leo (Swahili)
taifaleo.nation.co.ke
Read full article

Summary generated from the RSS feed of Taifa Leo (Swahili). All article rights belong to the original publisher. Click through to read the full piece on taifaleo.nation.co.ke.