“WAKAZI wa maeneo mbalimbali ya Pwani wanaishi kwa hofu huku maji ya Bahari ya Hindi yakizidi kuingia katika makazi yao, kuharibu mashamba, kubomoa majengo na kuwalazimu baadhi yao kuhama. Katika kijiji cha Mikokoni, Matsangoni, Kaunti ya Kilifi, Bw Charo Chome amekuwa akijenga ukuta mdogo kwa fedha kidogo anazopata mara kwa mara, akijaribu kuzuia bahari isiingie katika boma lake. Ukuta huo, ambao haujakamilika, umejengwa mahali ambapo zamani kulikuwa na shamba lake la minazi. Hata hivyo, maji ya chumvi tayari yameharibu mazao yake na kufunika sehemu kubwa ya ardhi yake. “Bahari imechukua karibu ekari tatu za ardhi yangu. Zamani maji hayakufika hapa. Kila nipatapo pesa kidogo naongeza sehemu ya ukuta huu, lakini sina uwezo wa kuumaliza,” alisema. Anasema hali hiyo ilianza miaka ya 1970 kwa mafuriko ya msimu yaliyokuwa mbali na makazi yake, lakini sasa maji yamekaribia nyumba yake kiasi kwamba hata choo chake hujaa maji kutoka chini ya ardhi. Wakazi wengine wa eneo hilo pia wameathirika. Mashamba mengi yamejaa maji ya chumvi na hayawezi tena kutumika kwa kilimo. Baadhi ya wakazi wameanza kuvuna chumvi kama njia mbadala ya kujikimu. Bi Saumu Tunje, mkazi wa Mikokoni, alisema mawimbi makubwa hugeuza baadhi ya vijiji kuwa visiwa. “Njia za kupita hufungwa na maji. Watu hushindwa kuvuka kwa miguu na shughuli za kawaida husimama,” alisema. Wataalamu wanaeleza kuwa hali hiyo husababishwa na mawimbi makubwa yanayotokea mara mbili kila mwezi wakati jua, mwezi na dunia vinapolingana, hali inayochochea kupanda kwa kina cha bahari. Ripoti ya Hali ya Hewa ya Kenya ya mwaka 2025, ilionya kuwa kiwango cha maji ya bahari katika pwani ya Kenya kinaendelea kuongezeka huku mawimbi makubwa yakishuhudiwa mara kwa mara. Katika Kaunti ya Lamu, hali si tofauti. Bw Omar Bakari Mohamed, maarufu kama Omar Juju, anasema maisha katika kijiji cha Kitangani, Mokowe, yamebadilika kabisa kutokana na kuongezeka kwa maji ya bahari. “Wakati mwingine unaamka asubuhi na kukanyaga maji ndani ya nyumba bila kujua yalifurika usiku. Mke na watoto wangu walihama kwa sababu si salama kuishi hapa,” alisema. Anasema majirani wengi wameondoka huku nyumba zikiharibiwa na maji ya chumvi. Sehemu iliyokuwa mkondo mdogo wa maji sasa imegeuka kuwa bwawa kubwa la maji ya bahari. Katika Kaunti ya Tana River, wakazi wa eneo la Kipini wamepoteza mali ya thamani kutokana na bahari. Hoteli maarufu ya Tana Lodge, iliyowekezwa zaidi ya Sh60 milioni miaka ya 1990, ilibomolewa kabisa na mawimbi ya bahari. Wakazi wanasema serikali za kaunti na kitaifa zimekuwa zikiahidi suluhu kama ujenzi wa kuta za bahari, lakini hadi sasa hakuna hatua madhubuti iliyochukuliwa. Mombasa nayo imeathirika. Kwenye ngome ya kihistoria ya Fort Jesus, mawimbi yalikuwa yakigonga msingi wa jengo hilo hadi kusababisha nyufa. Hali hiyo ililazimu ujenzi wa ukuta wa bahari mwaka 2018 ili kulinda eneo hilo. Hata hivyo, wataalamu wa mazingira wanaonya kuwa kuta za bahari pekee hazitoshi kukabili athari za mabadiliko ya tabianchi. Wanapendekeza kurejeshwa kwa mikoko na miamba ya matumbawe, pamoja na mipango bora ya matumizi ya ardhi na makazi salama kwa jamii zilizo hatarini.
Original story
Continue reading at Taifa Leo (Swahili)
taifaleo.nation.co.ke
Summary generated from the RSS feed of Taifa Leo (Swahili). All article rights belong to the original publisher. Click through to read the full piece on taifaleo.nation.co.ke.
