“TAHARUKI inaendelea kutanda katika Kaunti ya Kilifi kutokana na tishio la usalama baada ya makundi ya uhalifu kuendelea kutishia wakazi, biashara na sekta ya utalii. Viongozi wamejitokeza kukashifu kudorora kwa usalama wakiitaka idara ya usalama kudhibiti hali ambayo inazidi kuzorota. Gavana wa Kilifi, Bw Gideon Mung’aro, ambaye aliongoza kikao cha kiusalama baada ya kuongezeka kwa visa vya utovu wa nidhamu na hofu ya usalama katika kaunti hiyo, aliwataka viongozi kuimarisha ushirikiano na serikali, vyombo vya usalama, na kuandaa baraza za umma ili kuelimisha wakazi kuhusu jukumu muhimu la polisi kwa jamii katika kudhibiti usalama mitaani. Katika kikao hicho kilichoongozwa na Kamanda wa Polisi wa Ukanda, Bw Ali Nuno, Kamati ya Usalama ya Kaunti ya Kilifi, wabunge wa Kilifi akiwemo Bw Owen Baya (Kilifi Kaskazini) na mwenzake wa Malindi, Bi Amina Mnyazi, waliamua kushirikiana ili kuhakikisha kuna usalama Kilifi. “Tumejadili matukio ya hivi karibuni na kuongezeka kwa hofu ya usalama, na tumekubaliana kwa pamoja kuimarisha operesheni za usalama katika maeneo yote yaliyoathirika yakiwemo Malindi, Gede, Kakuyuni, Mayungu, Mtwapa, Mji wa Kilifi na makazi mengine ya Kaunti,” alisema Gavana Mung’aro. Bw Mung’aro alisema serikali yake imejitolea kushirikiana na maafisa wote wa usalama kuhakikisha utulivu unarejea. Bw Baya, alisema viongozi na vyombo vya usalama wameweka mikakati kabambe ya kukabiliana na hali ya usalama inayozorota katika kaunti hiyo. Alisema mkutano huo ulilenga kupanga na kuimarisha operesheni za usalama ili kudhibiti makundi ya wahalifu. “Tumekutana na vyombo vya usalama kupanga na kuweka mikakati ya kuboresha hali ya usalama inayozorota. Tutakabiliana na magenge ya wahalifu. Mawoza, wabakaji na wahalifu hawatatuendesha, tutawakabili ipasavyo,” alisema Bw Baya akisisitiza kuwa usalama wa wakazi wa Kilifi ni kipaumbele na akahimiza ushirikiano wa karibu kati ya wananchi na vyombo vya usalama ili kuhakikisha usalama. Aliyekuwa Waziri wa Jinsia, Bi Aisha Jumwa alisema suala la usalama linazidi kuwasumbua wakazi wa Kilifi. “Suala la usalama limekuwa tishio na kero kwa wakazi wa Kilifi. Lakini vyombo vya usalama vinaendelea na operesheni madhubuti ya kurejesha amani na usalama, na havitayumbishwa wala kuzuiwa kutekeleza wajibu wao,” alisema Bi Jumwa. Aliwasihi wananchi kuwapa maafisa wa usalama nafasi ya kufanya kazi yao ili kuwaondoa wahalifu hao. “Hatutakubali jamii yetu kuendelea kuishi kwa hofu kutokana na vitendo vya kihalifu. Sheria itachukua mkondo wake dhidi ya yeyote atakayehusika na uhalifu. Tutapigana na wahuni,” alisema Bi Jumwa.
Original story
Continue reading at Taifa Leo (Swahili)
taifaleo.nation.co.ke
Summary generated from the RSS feed of Taifa Leo (Swahili). All article rights belong to the original publisher. Click through to read the full piece on taifaleo.nation.co.ke.
