skipToContent
🌐All

Wanafunzi 2,000 wanufaika kupitia kliniki ya macho

Wanafunzi 2,000 wanufaika kupitia kliniki ya macho
KATIKA Kaunti ya Siaya ambako wanafunzi wengi wamekuwa wakikata kiu cha masomo kwenye mazingira yenye changamoto, huduma za ukaguzi wa macho zimeanza kubadilisha maisha yao. Kwa karibu wanafunzi 2,000 kutoka shule za St. Albert’s Simero Mixed, Rang’ala Boys High na Rang’ala Primary, kliniki ya bure ya macho iliyoandaliwa na Baraza la Kenya la Watu Wanaoishi na Matatizo ya Kuona, ndio, Kenya Society for the Blind kwa ufadhili wa Rural Electrification and Renewable Energy Corporation (REREC) haikutoa tu huduma ya matibabu, bali pia ilirejesha matumaini, kujiamini na uwezo wao wa kuona vizuri. Kwa miaka mingi, baadhi ya wanafunzi kutoka eneo hilo walikuwa wakikumbwa na matatizo ya kuona yaliyokuwa yakiathiri masomo yao kimyakimya. Wengine walishindwa kusoma maandishi yaliyoandikwa ubaoni, huku wengine wakisumbuliwa na maambukizi ya macho ya mara kwa mara bila kuelewa chanzo chake. Aghalabu, walimu walichukulia hali hiyo kama uzembe, ukosefu wa umakini au kutokuwa makini darasani. Mpango huo wa wiki moja uliongozwa na Dkt Albert Macua, Mkuu wa Huduma za Macho na Uhamasishaji wa Afya katika Kenya Society for the Blind. Ukaguzi ulionyesha kuwa tatizo kubwa zaidi miongoni mwa wanafunzi hao lilikuwa shida za kuona zinazoweza kurekebishwa kwa miwani maalum. “Duniani kote, matatizo hayo ni miongoni mwa visababishi vikuu vya uonaji hafifu na upofu, hasa kwa watoto wa shule. Hata hivyo, wataalamu wa afya wanasema hali hiyo inaweza kurekebishwa kwa urahisi iwapo itagunduliwa mapema,” akasema Dkt Macua. Miongoni mwa walionufaika alikuwa Jayden Ochieng, mtoto mwenye mahitaji maalum. Mama yake, Catherine Achieng, alisema aliguswa sana baada ya kufahamishwa kuwa mwanawe alihitaji miwani maalum ili kuboresha uwezo wake wa kuona. Kwa muda mrefu, alikuwa akitazama mwanawe akihangaika kutekeleza shughuli za kawaida bila kuelewa tatizo lilikuwa nini. “Sikuwahi kufikiria kuwa tatizo la macho lilikuwa sehemu ya changamoto zinazomkabili mwanangu,” Bi Achieng alisema. “Leo hii, nina furaha sana kwa sababu sasa ana nafasi ya kuishi na kujifunza vizuri zaidi kama watoto wengine.” [caption id="attachment_188153" align="aligncenter" width="300"] Meneja Mkuu wa Habari, Elimu na Mawasiliano wa REREC, Beatrice Njuguna, taasisi ya kawi inayoendeleza huduma za ukaguzi wa macho kupitia mipango yake ya kijamii. Picha|Hisani [/caption] Kulingana na Mratibu wa Huduma za Macho katika Kaunti ya Siaya, Calvin Omondi, upatikanaji wa huduma za macho bado ni changamoto kubwa katika maeneo mengi ya gatuzi hilo. Alisema watu wengi wanaishi na matatizo ya macho bila kupata matibabu kwa sababu ya ukosefu wa pesa, raslimali, wataalamu na uelewa wa kutosha. “Katika jamii nyingi za vijijini, watoto wanaendelea kuishi na matatizo ya macho ambayo hayajatibiwa kwa sababu wazazi hawawezi kugharamia matibabu au hawajui tatizo lilipo,” Omondi alisema. Aliongeza, “Ndio maana ushirikiano kati ya mashirika kama REREC na Kenya Society for the Blind ni muhimu sana katika jamii.” Wataalamu wa afya ya macho wanakadiria kuwa maelfu ya Wakenya wanaishi na upofu au matatizo ya kuona yanayoweza kuzuilika. Baadhi ya matatizo hayo yanahusishwa na jicho kukumbwa na ‘wingu’, kwa Kiingereza cataract , hitilafu za kuona, glaucoma, pamoja na maambukizi yasiyotibiwa kwa wakati ufaao. Aidha, watoto huathirika zaidi kwa sababu mara nyingi matatizo ya kuona hugunduliwa tu baada ya mtoto kushusha umahiri wa kusoma au matokeo kuwa duni. Kwa miaka kadhaa sasa, Kenya Society for the Blind imekuwa ikihamasisha jamii kuhusu afya ya macho kupitia uchunguzi na ukaguzi bila malipo, usambazaji wa miwani maalum na msaada kwa watu wenye ulemavu wa kuona kote nchini. Kwa upande wa Rural Electrification and Renewable Energy Corporation, taasisi hiyo ya kawi imekuwa ikiunganisha miradi ya afya na elimu katika programu zake za kuinua jamii. Akizungumza kuhusu mpango huo, Meneja Mkuu wa Habari, Elimu na Mawasiliano wa REREC, Beatrice Njuguna, alisema kliniki hiyo ya macho ililenga kuboresha maisha ya wanafunzi kutoka jamii zisizo jiweza. “Mpango huu unaonyesha uhusiano mkubwa kati ya afya na elimu, kwa sababu mtoto hawezi kujifunza vizuri ikiwa hana uwezo mzuri wa kuona,” alisema. Ziara ya Siaya shuleni ilikuwa kliniki ya nne ya macho kuandaliwa na REREC baada ya programu kama hizo kufanyika katika kaunti za Kirinyaga, Taita Taveta na Kitui.
Share
Original story
Continue reading at Taifa Leo (Swahili)
taifaleo.nation.co.ke
Read full article

Summary generated from the RSS feed of Taifa Leo (Swahili). All article rights belong to the original publisher. Click through to read the full piece on taifaleo.nation.co.ke.