“WANAHARAKATI wa haki za binadamu wanaopinga kutimuliwa kwa aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua wameanzisha mashambulizi makali ya kikatiba dhidi ya Bunge na Serikali. Katika mawasilisho yao ya mwisho mbele ya majaji watatu Ijumaa, walalamishi wenza 40 walisema kuruhusu kutimuliwa kwa Bw Gachagua kudumu kutadhoofisha ulinzi wa kikatiba, kuhalalisha njia za mkato za kisiasa na kuirudisha Kenya katika enzi za matumizi mabaya ya mamlaka kabla ya Katiba ya 2010. Walionya kuwa Bunge lilibadilisha mchakato wa kumuondoa aliyekuwa Naibu Rais kuwa “hesabu za kisiasa” badala ya mchakato wa kikatiba. Walimuunga mkono Bw Gachagua katika ombi lake la kutaka mahakama itangaze kuwa kuondolewa mamlakani kwake kulikuwa kinyume cha Katiba na anafaa kulipwa fidia. Kesi hiyo sasa imekuwa mojawapo ya mapambano muhimu zaidi ya kikatiba nchini tangu kupitishwa kwa Katiba ya 2010. Kiini cha mzozo huo ni iwapo Bunge la Kitaifa na Seneti zilimuondoa Bw Gachagua afisini kwa njia halali Oktoba 2024 kabla ya Rais William Ruto kumteua Profesa Kithure Kindiki kuwa Naibu Rais. Walalamishi wanasisitiza kuwa mchakato wa kumtimua mamlakani ulikiuka haki za kusikilizwa kwa haki, ushirikishaji wa umma, utaratibu unaostahili na ugavi wa mamlaka. Wakili Evans Ogada aliambia majaji kuwa mahakama haziwezi kukataa kuchunguza mchakato wa kuondolewa mamlakani kwa madai kwamba ni suala la kisiasa. “Katiba ya Kenya ni ya mageuzi na ilipunguza nguvu za utawala wa kiimla,” alisema. “Masuala yote, hata ya kisiasa, yanaweza kuchunguzwa na mahakama.” Bw Ogada alikosoa hoja za Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Seneti na Bunge la Kitaifa zilizotegemea kile kinachoitwa “ itikadi za kisiasa ”, akisema Katiba iliunda mahakama yenye mamlaka ya kusimamia matumizi yote ya mamlaka ya umma. “Ikiwa mahakama zitakataa kuamua kesi za kisiasa, zitakuwa zimeacha wajibu na mamlaka zilizopewa na Katiba,” alisema. Wakili huyo alisema kuondolewa mamlakani ni mchakato wa kisheria unaotawaliwa na ulinzi mkali wa kikatiba na si kura za kisiasa. “Katiba hairuhusu kuondolewa kwa msingi wa shinikizo au hesabu za kisiasa. Mahakama hii ndiyo mlinzi wa Katiba,” alisema. Mawasilisho hayo yalijiri siku chache baada ya mawakili wa Naibu Rais Kithure Kindiki kuonya kuwa kubatilishwa kutimuliwa kwa Gachagua kunaweza kusababisha mgogoro wa kikatiba na kuifanya Kenya kuwa na “manaibu rais wawili”. Lakini wakili Kibe Mungai alipuuza madai hayo na kuwataka majaji kuzingatia tu iwapo Katiba ilifuatwa. “Hakutakuwa na mgogoro wowote wa kikatiba ikiwa mahakama itabatilisha kuondolewa kwa Gachagua,” alisema. Walalamishi pia walishutumu Bunge kwa kutumia taratibu za kumuondoa rais madarakani katika kumtimua Naibu Rais bila kurekebisha mfumo huo kulingana na mahitaji ya kikatiba. Bw Mungai alisema Bunge la Kitaifa na Seneti hazina kanuni maalumu za kusimamia kuondolewa mamlakani kwa Naibu Rais. “Hawawezi kuondoa kiongozi mamlakani bila utaratibu maalumu. Kesi ya Gachagua ilikuwa mzaha,” alisema. Mawakili Njeri Maina na Andrew Muge walidai kuwa Bunge lilichanganya majukumu ya uchunguzi, mashtaka na kutoa uamuzi katika mchakato huo. “Lazima kuwe na mipaka ya matumizi ya mamlaka ya Bunge,” waliambia majaji. Walalamishi walisisitiza kuwa mahakama zina mamlaka ya kuchunguza sio tu taratibu bali pia msingi wa kuondolewa mamlakani. Mawakili Ndegwa Njiru, Omoke Morara na Sasha Wamae pia walishambulia uteuzi wa Profesa Kindiki kuwa Naibu Rais wakisema wananchi hawakushirikishwa katika kujaza nafasi hiyo. “Wananchi wa Kenya hawakushirikishwa katika kujaza nafasi ya Gachagua,” waliwasilisha. Walidai kuwa mchakato wa kuidhinisha Profesa Kindiki ulifanywa kwa haraka usiku bila ushirikishaji wa maana wa umma. Kesi hizo zilizounganishwa zinasikizwa na Majaji Eric Ogolla, Anthony Mrima na Frida Mugambi.
Original story
Continue reading at Taifa Leo (Swahili)
taifaleo.nation.co.ke
Summary generated from the RSS feed of Taifa Leo (Swahili). All article rights belong to the original publisher. Click through to read the full piece on taifaleo.nation.co.ke.
