skipToContent
🌐All

Wanakijiji walalamikia moshi hatari kutoka hospitalini

Taifa Leo (Swahili) Global
Wanakijiji walalamikia moshi hatari kutoka hospitalini
WANAKIJIJI wa Hidabo kisiwani Lamu wanahofia athari za kiafya kutokana na moshi na harufu kali kutoka kwenye tanuri ya kuchomea taka za kimatibabu hospitalini. Kijiji cha Hidabo ni makazi ya zaidi ya watu 500 na kinapakana na hospitali kuu ya rufaa ya King Fahd, ambayo ndiyo kubwa zaidi kaunti ya Lamu. Bi Fatma Alwy, mkazi, anasema moshi wa harufu mbaya wenye mchanganyiko wa kemikali unaowafikia kwenye makazi yao kutoka kwa mtambo huo umesababishia wengi wao maradhi na matatizo ya kupumua. “Nilitembelea hospitali hivi majuzi baada ya kuhisi kifua changu ni kizito na kubana. Baada ya kukaguliwa niliarifiwa kwamba nina pumu. Katika ukoo wetu hatujaugua maradhi kama hayo. Naamini ilichangiwa na moshi kutoka kwa tanuri la kuchomea taka za hospitali,” akasema Bi Alwy. Mzee wa kijiji cha Hidabo, Bw Swaleh Babu, alisema wakazi wengi wamejitokeza kulalamikia moshi na harufu mbaya kijijini kutoka kwa mtambo huo. Alitilia shaka kama tathmini yoyote ya athari ya mazingira ilifanywa na mamlaka husika inavyotakikakana kisheria kabla tanuri hiyo kujengwa. “Watoto wetu wanakohoa mara kwa mara. Yote yamechochewa na moshi kutoka kwa tanuri ya hospitali. Inazalisha hewa chafu yenye mchanganyiko wa kemikali. Kila tukivuta hewa tunatatizika hapa kijijini,” akasema Bw Babu. Aliongeza, “Twahisi kihamishwe au zibuniwe mbinu mpya za kudhibiti huo.” Bi Mariam Hamisi, ambaye makazi yake ni ya ghorofani kijijini Hidabo, anasema kila mara mtambo unapowashwa, moshi husambaa na kuingia moja kwa moja mpaka ndani ya nyumba yake. “Unapata sisi tunaoishi juu kushinda hilo tanuri twateseka. Ni wajibu wa wasimamizi kulirefusha ili liende juu hewani kabisa kuzuia moshi kuishia kusambaa makazini mwetu tusiathirike. Tunalazimika kufunga madirisha na milango ya nyumba zetu tukiwa ndani ambalo si jambo zuri,” akasema Bi Hamisi. Moshi unaozalishwa kutoka kwa tanuri hilo pia umetajwa kuathiri pakubwa afya ya wanawake wajawazito. Mtetezi wa haki za binadamu na jamii ya Hidabo Ahmed Famau, aliitaka serikali kuanzisha mchakato wa kuwapokeza matibabu ya bure wakazi wa Hidabo kutokana na maradhi waliyoambukizwa kupitia tanuri la kuchomea taka za hospitali. Pia aliwataka wahusika kuwafidia wakazi kwa kuwasababishia madhara. Naibu Gavana wa Lamu, Dkt Mbarak Salim, ambaye pia ni Waziri wa Afya wa kaunti, alikiri kuwa tanuri hilo limekuwa na matatizo ya kutoa moshi lakini likarekebishwa hivi majuzi. Dkt Salim hata hivyo alikosoa pendekezo la wananchi kwamba mtambo huo uhamishiwe kwingine. “Walikuta hospitali na mtambo ukiwa tayari unaendeleza majukumu yake pale. Walijenga makazi yao Hidabo bila kufuata kanuni zifaazo,” akasema Dkt Salim. Afisa mtaalamu wa mazingira, Bw Dickson Mbuthia, alihimiza hospitali nchini kutumia mbinu salama wakati wanapotekeleza uchomaji wa taka na mabaki ya vifaa vya matibabu. Alionya kuwa hewa chafu, na kemikali zikienea hewani mara nyingi huishia kuathiri binadamu. “Watu pia huishia kupata kikohozi, kupumua kwa shida na vifua kubana. Lazima tujukumike kwa kuhakikisha mitambo yote ya kuchoma taka hospitalini inafanya kazi bila kuhatarisha afya za jamii na mazingira yetu,” akasema Bw Mbuthia.
Share
Original story
Continue reading at Taifa Leo (Swahili)
taifaleo.nation.co.ke
Read full article

Summary generated from the RSS feed of Taifa Leo (Swahili). All article rights belong to the original publisher. Click through to read the full piece on taifaleo.nation.co.ke.