“TAKRIBAN watu 90 walifariki kufuatia mlipuko katika mgodi wa makaa ya mawe [coal kwa Kimombo] kaskazini mwa China, kulingana na vyombo vya habari vya serikali ya nchi hiyo. Mlipuko huo wa gesi ulitokea katika Mgodi wa Makaa ya Mawe wa Liushenyu unaomilikiwa na kampuni ya Tongzhou Group katika Mkoa wa Shanxi. Mamia ya waokoaji walitumwa katika eneo hilo huku watu 27 wakiripotiwa kulazwa hospitalini wakipokea matibabu, mmoja akiwa katika hali mahututi. Operesheni za uokoaji bado zinaendelea. Mlipuko huo ulitokea usiku Ijumaa katika mgodi huo uliokuwa na wafanyakazi 247 waliokuwa kazini wakati wa ajali hiyo. Mmoja wa wachimbaji waliojeruhiwa, Wang Yong, aliambia televisheni ya serikali kuwa hakusikia mlio wowote wakati mlipuko ulipotokea bali aliona moshi mzito ukitanda ghafla. “Nilinusa harufu kama ile ya milipuko. Nikaanza kuwapigia watu kelele wakimbie. Tulipokuwa tunakimbia niliona watu wakianguka kutokana na moshi huo. Baadaye nami nikapoteza fahamu,” alisema. Aliongeza kuwa alikaa chini kwa karibu saa moja kabla ya kuzinduka na kumwamsha mwenzake waliyetoroka pamoja kutoka mgodini. Baada ya mkasa huo, Rais wa China Xi Jinping aliagiza juhudi zote zifanywe kuwahudumia majeruhi na kutafuta manusura. Pia aliitaka serikali kuchunguza chanzo cha ajali hiyo na kuwachukulia hatua waliohusika. Vyombo vya habari vya serikali vilisema maafisa wanaosimamia mgodi huo wamezuiliwa huku uchunguzi ukiendelea. Hata hivyo, chanzo rasmi cha mlipuko huo bado hakijatangazwa. Ripoti zinaonyesha viwango vya gesi ya kaboni, ambayo ni sumu kali isiyo na harufu, vilipatikana kuwa juu ya kiwango kinachoruhusiwa. Wizara ya Usimamizi wa Dharura ya China ilituma wafanyakazi 345 kutoka vikosi sita vya uokoaji kusaidia shughuli hizo. Mnamo mwaka 2024, mgodi wa Liushenyu ulitajwa na Mamlaka ya Kitaifa ya Usalama wa Migodi ya China kuwa miongoni mwa migodi yenye “hatari kubwa za usalama”. Kampuni ya Tongzhou Group pia ilipewa adhabu mbili za kiutawala mwaka 2025 kutokana na masuala ya usalama. Mkoa wa Shanxi huzalisha zaidi ya robo ya makaa yote ya mawe nchini China. Ingawa viwango vya usalama katika sekta hiyo vimeimarishwa katika miaka ya hivi karibuni, ajali za migodini bado hutokea mara kwa mara. Mwaka 2023, watu 53 walifariki baada ya mgodi wa wazi kuporomoka katika eneo la Inner Mongolia kaskazini mwa China. Mwaka 2009, zaidi ya watu 100 waliuawa katika mlipuko mwingine wa mgodi katika Mkoa wa Heilongjiang kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.
Original story
Continue reading at Taifa Leo (Swahili)
taifaleo.nation.co.ke
Summary generated from the RSS feed of Taifa Leo (Swahili). All article rights belong to the original publisher. Click through to read the full piece on taifaleo.nation.co.ke.
