“WIZARA ya Usalama wa Ndani na Utawala wa Kitaifa imeanzisha mpango wa Sh20 bilioni wa kupanua Kituo cha Kitaifa cha Ulinzi na Udhibiti wa Usalama (IC4), pamoja na mageuzi mengine yanayolenga kuimarisha uwezo wa polisi kushughulikia uchaguzi mkuu wa mwaka 2027. Katibu wa Usalama wa Ndani, Dkt Raymond Omollo, aliambia Kamati ya Bunge kuhusu Utawala wa Kitaifa na Usalama wa Ndani, kuwa mpango huo wa kuboresha huduma za polisi utaimarisha uwezo wa maafisa katika ufuatiliaji wa matukio, kukabiliana na dharura na kudhibiti umati kabla ya uchaguzi. Mpango huo unatarajiwa kukamilika ifikapo Juni mwaka ujao, miezi miwili pekee kabla ya uchaguzi mkuu. Serikali imesema hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha sekta ya usalama iko tayari kukabiliana na hali yoyote wakati wa uchaguzi. Akizungumza mbele ya Kamati ya Bunge kuhusu makadirio ya bajeti ya mwaka wa fedha 2026/2027, Dkt Omollo alisema mfumo mpya wa IC4 utapanua mtandao wa sasa wa kamera na vifaa vya usalama kutoka Nairobi na Mombasa hadi Kisumu, Eldoret, Nakuru na Nyeri. Katika mpango huo mpya, kutakuwa na mfumo wa uchambuzi wa kisasa wa taarifa, vitabu vya kidijitali vya matukio ya polisi (OB) pamoja na mfumo unaowaunganisha machifu na wasimamizi wa serikali katika mfumo mmoja wa kitaifa wa usalama. “Makadirio ya gharama ya mradi huu ni takriban Sh20 bilioni na tunatarajia utekelezaji wake kukamilika ndani ya mwaka mmoja ili kufikia Juni mwaka ujao, kabla ya uchaguzi, uwe umeanza kufanya kazi kikamilifu,” Dkt Omollo aliwaambia wabunge. Alieleza kuwa fedha hizo zitatumika kuboresha na kubadilisha mradi wa zamani wa IC3 ulioanzishwa mwaka 2013 na ambao muda wake wa matumizi tayari umeisha. Kwa upande wake, Inspekta Jenerali wa Polisi, Bw Douglas Kanja, alisema idara hiyo iko tayari kuhakikisha Wakenya wanashiriki uchaguzi wa amani mwaka 2027. “Tuko tayari kwa maandalizi kwa sababu tumewahi kufanya hivi awali. Tulifanya wakati wa uchaguzi wa 2022 na matokeo yake yanaonekana. Tutafanya tena mwaka 2027,” Bw Kanja alisema. Aliwaambia wabunge kuwa uchaguzi ni msingi muhimu wa demokrasia ya Kenya na kwamba polisi wana wajibu wa kikatiba wa kuhakikisha wananchi wanatekeleza haki zao za kidemokrasia kwa amani. “Mafunzo ni muhimu sana. Tunahitaji maafisa wetu wote wawe tayari kuhusu masuala ya uchaguzi, ikiwemo usimamizi wa utulivu wa umma. Usaidizi wa kamati hii utatusaidia kuimarisha maandalizi yetu,” alisema. Bw Kanja alisema mfumo mpya wa IC4 utarahisisha kazi ya polisi katika kukabiliana na watu wanaopanga kuzua vurugu wakati wa uchaguzi. “Matumizi ya teknolojia katika kazi za polisi, ikiwemo kamera zinazovaliwa mwilini, yatatoa ushahidi muhimu na pia kusaidia kutambua maafisa wanaotuhumiwa kwa uongo,” alisema. Hata hivyo, baadhi ya wabunge walieleza wasiwasi kuhusu uwazi wa matumizi ya fedha, maswali ya ukaguzi wa hesabu na kuongezeka kwa matumizi wakati taifa likikabiliwa na changamoto za kiuchumi. Mbunge wa Loima, Bw Protus Akuja alihoji ukosefu wa maelezo ya kina kuhusu ununuzi wa vifaa, muda wa utekelezaji wa mradi huo na majukumu ya kifedha yatakayojitokeza baadaye. “Tunahitaji ufafanuzi kamili kuhusu gharama ya mradi, ununuzi wa vifaa, ratiba ya utekelezaji na fedha zitakazohitajika baadaye ili kuhakikisha uwazi na kuepuka ongezeko la gharama,” alisema. Dkt Omollo pia alifichua kuwa baadhi ya helikopta zilizokwama katika kitengo cha anga cha polisi ni sehemu ya mpango wa serikali kabla ya uchaguzi wa 2027. “Nathibitisha kuwa helikopta ni sehemu ya mpango huu. Pia tunakusudia kukarabati helikopta moja kusaidia shughuli za polisi,” alisema. Kulingana na Katibu huyo, mpango huo pia utahusisha ununuzi wa vifaa vya kudhibiti ghasia, droni, magari na risasi ili kuimarisha uwezo wa polisi wakati wa shughuli nyingi za kisiasa. Dkt Omollo aliomba kamati hiyo kuidhinisha ombi lao la nyongeza ya Sh22.8 bilioni licha ya bajeti ya matumizi ya kawaida kupunguzwa kutoka Sh48.2 bilioni mwaka huu hadi Sh45.7 bilioni katika mwaka wa fedha wa 2026/2027. Alikiri kuwa kupunguzwa kwa fedha kutaathiri shughuli za polisi wakati taifa linajiandaa kwa uchaguzi mkuu wa 2027.
Original story
Continue reading at Taifa Leo (Swahili)
taifaleo.nation.co.ke
Summary generated from the RSS feed of Taifa Leo (Swahili). All article rights belong to the original publisher. Click through to read the full piece on taifaleo.nation.co.ke.
