skipToContent
UAEAll

Yuko wapi Oburu? Maswali tele kuhusu aliko kinara wa ODM akipitwa na hafla nyingi

Yuko wapi Oburu? Maswali tele kuhusu aliko kinara wa ODM akipitwa na hafla nyingi
KIONGOZI wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM), Oburu Oginga, hajaonekana katika hafla muhimu za chama hicho katika siku za hivi karibuni, hali iliyozua uvumi mkali kuhusu mahali alipo na afya yake. Uvumi huo ulianza kuenea takriban wiki mbili zilizopita lakini ulipata nguvu zaidi baada ya Dkt Oginga kukosa kuhudhuria mkutano mkubwa wa chama uliofanyika Mombasa wiki iliyopita, mkutano uliohudhuriwa na viongozi wakuu wa ODM pamoja na mawaziri na magavana waliochaguliwa kwa tiketi ya chama hicho. Mkutano huo uliwaleta pamoja magavana wa ODM, wabunge, wanachama wa Kamati Kuu ya Kitaifa (NEC) pamoja na mawaziri John Mbadi (Fedha), Hassan Joho (Madini) na Wycliffe Oparanya (Ushirika). Hata hivyo, kutohudhuria kwa kiongozi huyo mkuu kuliibua maswali ndani na nje ya chama. Kwa mujibu wa rekodi za hafla za ODM, Dkt Oginga alionekana mara ya mwisho katika shughuli ya kisiasa Aprili 20 alipohudhuria mkutano wa vijana wa chama hicho uliofanyika Nairobi. Tangu wakati huo, amekosa mikutano kadhaa muhimu ya chama, ukiwemo mkutano kama huo uliofanyika Kilifi Aprili 26. Kutohudhuria kwake pia kumeonekana katika hafla za kitaifa zenye uzito mkubwa. Gavana wa Mombasa Abdulswamad Nassir alilazimika kuzindua Hospitali ya Raila Odinga mjini Nyali bila kuwepo kwa kiongozi wa chama, licha ya tukio hilo kuwa na uzito mkubwa wa kisiasa na kihistoria kwa ODM. Aidha, Dkt Oginga alikosa mazishi ya Mzee Edwin Kipchirchir Koech, baba wa Waziri wa Uchukuzi Davis Chirchir, yaliyohudhuriwa na Rais William Ruto pamoja na viongozi wakuu wa serikali na ODM. Wakati huo huo, alikosa pia sherehe za Siku ya Wafanyakazi (Leba Dei) zilizofanyika Vihiga, pamoja na mazishi ya Mzee Eliud Nyikal Okaka, katika eneo la Seme, Kisumu, ambapo viongozi wengi wa ODM walihudhuria. Katika mazishi ya Seme, magavana wote wa eneo la Nyanza walikuwepo, akiwemo Gladys Wanga, Anyang Nyong'o, James Orengo na Ochillo Ayacko, jambo lililoongeza zaidi mjadala kuhusu afya na mahali alipo kiongozi huyo. Wasiwasi ulizidi kuongezeka zaidi baada ya kukosa mkutano wa Mombasa uliochukua siku mbili. Kabla ya mkutano huo, kulikuwa na mazungumzo ndani ya chama kupendekeza uahirishwe ili kumpa nafasi Dkt Oginga ahudhurie, lakini uamuzi ulifanywa uendelee ilivyopangwa. Katika mkutano huo, hotuba yake ilisomwa na naibu kiongozi wa chama, Gavana wa Kisii Simba Arati. Katika ujumbe wake, Oginga aliomba radhi kwa kutokuwepo, akieleza kuwa alikumbwa na “hali zisizotarajiwa na zisizoweza kuepukika.” “Nilikuwa nimepanga kuhudhuria mkutano huu muhimu, lakini kutokana na hali zisizotarajiwa na zisizoweza kuepukika nimekosa kuhudhuria,” ilisoma sehemu ya hotuba yake. Ndani ya chama, duru za kuaminika zilieleza kuwa kiongozi huyo alikuwa akipata mapumziko nyumbani kwake Nairobi kwa ushauri wa daktari wake, jambo lililochochea zaidi uvumi wa afya yake. Hata hivyo, Mbunge wa Suna, Junet Mohammed alikanusha uvumi huo akisema Dkt Oginga yuko katika afya nzuri na anatarajiwa kurejea kazini hivi karibuni. Alithibitisha pia kuwa kiongozi huyo anatarajiwa kuongoza mkutano wa Kamati Kuu ya Chama wiki ijayo. “Yuko sawa kabisa. Nimezungumza naye asubuhi hii. Tunapanga mkutano wa Kamati Kuu wiki ijayo,” alisema Junet. Katika miezi ya hivi majuzi, Dkt Oginga amekuwa akibeba mzigo mkubwa wa majukumu ndani ya ODM, chama ambacho sasa kinakabiliwa na migawanyiko ya kisiasa na kuibuka kwa makundi hasimu ndani yake. Dkt Oginga alichukua usukani ODM baada ya kifo cha ndugu yake, hatua iliyomuweka katikati ya siasa za kasi na mikutano ya mara kwa mara ya kuhusu mizozo. Mwaka jana, alienda likizoni Dubai kutokana na kile kilichoelezwa kuwa uchovu wa kisiasa na shinikizo za kazi, hali iliyozua pia mijadala kuhusu afya na mustakabali wake kisiasa.
Share
Original story
Continue reading at Taifa Leo (Swahili)
taifaleo.nation.co.ke
Read full article

Summary generated from the RSS feed of Taifa Leo (Swahili). All article rights belong to the original publisher. Click through to read the full piece on taifaleo.nation.co.ke.